DC Iringa akerwa mikutano ya kusikiliza kero

MKUU wa Wilaya ya Iringa, Kheri James ameonesha kutofurahishwa na mikutano inayohusu usikilizaji wa kero za wanachi akisema hiyo ni dalili ya baadhi ya mifumo ya utendaji serikalini kushindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa.

Amesema hayo wakati akifungua Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na kutangaza mpango wake wa kufanya ziara ya kata kwa kata mjini Iringa.

“Nimekamilisha ziara yangu kwa ngazi ya halmashauri na tarafa zote za wilaya ya Iringa, sasa natarajia kuanza ziara ya kata kwa kata na kwa kuanzia nitajielekeza katika kata zote za Iringa mjini,” amesema na kuongeza:

“Mimi ziara zangu hazitakuwa za kusikiliza kero, zitakuwa za kueleza makubwa yanayofanywa na serikali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan katika sekta mbalimbali na kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.”

Aliwageukia watendaji wote wa serikali katika wilaya yake hiyo akisema kero sio sifa na kwamba wanatakiwa kutimiza wajibu wao kwa kumaliza changamoto zote zinazotengeneza kero katika maeneo yao ya kazi.

“Tukiwa na huduma bora na utumishi uliotukuka, tunazingatia sheria, taratibu na kanuni tulizojiwekea na katika maeneo yetu yote ya kazi tunawasikiliza wananchi na kuzifanyia kazi kwa wakati hoja zao, hizo kero zinazotolewa kwa viongozi kwenye mikutano ya hadhara zitatoka wapi?” Amehoji.

Amesema wananchi wanatoa kero zao kwa viongozi kwa sababu mifumo ya utatuzi wa changamoto zao katika ngazi zinazohusika imekwama na hicho ni kishiria kwamba watendaji katika maeneo hayo hawana au wamepoteza sifa za kuwa watumishi wa watu.

Pamoja na kwamba ziara yake hiyo hailengi kusikiliza kero, James amesema atatumia fursa hiyo kuwasikiliza wananchi hatua itakayomuwezesha kubaini kata zenye kero nyingi na kupendekeza hatua za kuchukua kwa watendaji ambao ni sehemu ya changamoto katika maeneo yao.

Habari Zifananazo

Back to top button