DC Iringa awataka akinamama kuachana na ‘vibenteni’

MKUU wa Wilaya ya Iringa, Verronica Kessy amewaonya akina mama (wanawake watu wazima) wanaojihusisha kimapenzi na wavulana wadogo (vibenteni) akisema huo ni ukatili wa kingono dhidi ya watoto unaoangukia kwenye makosa ya ubakaji.

“Ukatili huu wa kingono hujumuisha vitendo ambavyo havihusishi sana vitendo vya kushurutisha au vitisho, bali ni vile ambavyo vinaweza kufanywa kwa njia ya maneno ya kubembeleza, hongo, utii, hadhi, mamlaka, na kupotosha desturi za kijamii,” alisema.

Akikemea matukio hayo kwenye maadhamisho ya siku ya Wanawake Duniani ambayo kiwilaya yamefanyika katika Kata ya Migoli wilayani Iringa, Kessy alisema katika mazingira hayo mhusika (mtoto) anaweza asitambue ukatili huo wa kingono unaofanywa dhidi yake.

“Kama nchi tunapaswa kuchukua hatua dhidi ya ukatili huu ambao pia uwaathiri sana watoto wa kike na kujumuisha kujamiiana kwa ndugu wenye uhusiano wa damu, ubakaji na ulawiti,” alisema huku akiwataka wadau kutoa taarifa za matukio ya aina hiyo ili mamlaka ziweze kuchukua hatua za kisheria.

Mkuu wa Wilaya amewasihi wazazi na walezi kuwa makini katika kusimamia malezi ya watoto wao kwa kujua michezo wanayocheza na aina ya marafiki wanaoambatana nao kwani jamii ya sasa imechafuka kimaadili.

“Wazazi na walezi tengeni muda wa kuzungumza na watoto wenu na msikubali watoto wenu walale na watu msiowaamini ili kuisaidia nchi kukabiliana na kukomesha ukatili wa kingono,” alisema.

Aidha amewatahadharisha wananchi kuwa makini na taasisi zinazotoa misaada akisema zipo baadhi yake (hakuzitaja) ambazo kwa kupitia elimu na misaada zinayotoa zimekuwa kwa namna moja au nyingine zikihamasisha mapenzi ya jinsia moja (Ushoga) kinyume na maadili ya mtanzania.

“Tuwe makini na picha zikiwemo za katuni, mafundisho na machapisho yoyote yale yanayohamasisha ushoga.

Zipo taarifa za kuwepo kwa baadhi ya watanzania wenzetu wana wanaoshiriki vitendo hivyo vya ushoga, hii ni kufuru kwa Mwenyezi Mungu, tupige goti tuombe vitendo hivi vitoweke” alisema.

Awali akitoa taarifa ya ukatili, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Loveness Mayingu alisema kasi ya matukio ya ulawiti mkoani Iringa inaongozeka huku waathirika zaidi wakiwa ni watoto wa kiume jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa kizazi kijacho.

“Pamoja na ujengaji wa uelewa kuhusu uhalifu huu, sambamba na kukamatwa na kutoa adhabu kwa wafanyaji wa makosa ya ukatili wa kingono dhidi ya watoto kunaweza kuwa na ushawishi wa faida juu ya desturi za tamaduni zetu,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button