DC Jokate awataka wananchi kuondoka vijiweni
MKUU wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo amewataka wananchi anaowaongoza kuondokana vijiweni na kuchangamkia fursa za ajira.
Jokate ameyasema hayo wakati akizindua bidhaa mpya ya unga wa Ngano wa PHF unaozalishwa na kampuni ya Azania Group.
Jokate ameeleza kuwa kampuni hiyo inatekeleza kwa vitendo sera ya Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuisaidia jamii katika mambo mbalimbali ikiwemo ajira ambayo imekuwa tatizo kubwa nchini.
“Kipekee kabisa naomba niushukuru uongozi wa Kampuni ya Azania Group kwa kuajiri idadi kubwa ya wafanya kazi kutoka katika wilaya yetu ya Temeke hili ni jambo jema na nipo tayari kuwasaidia endapo mtakuwa na jambo lolote lenye tija kwa taifa la Tanzania karibuni sana ofisini kwangu,” alisema Jokate.
Aidha aliipongeza Kampuni hiyo kwa kuzalisha bidhaa bora ya PHF, ambayo kwa kiasi kikubwa itawasaidia akina mama wajasiriamali ambao ndio watumiaji wakubwa wa bidhaa hiyo.
Alisema anatambua sokoni kuna changamoto nyingi na ushindani mkubwa lakini amewataka kuendelea kutumia weledi wao kwa kutengeneza bidhaa zenye ubora wa hali ya juu hiyo itawasaidia wao kuendelea kufanya vizuri ndani na nje ya Tanzania.
Kwa upande wake Joel Laiser ambaye ni Mkurugenzi wa biashara wa kampuni hiyo, alisema kuwa kabla ya kutoa unga huo walifanya tafiti ya kutosha na kugundua kero wanazozipata akina mama lishe katika biashara zao za kila.
“Unga huu ni laini na mweupe na kama ulikuwa nusu kilo unatoka chapati 10 sasa ujazo huo huo utatoa chapati zaidi ya hizo na kwa kweli hata bei zetu ni nafuu ambazo zinaendana na hali halisi ya Mtanzania wa hali ya chini,” alisema Laiser.