MKUU wa Wilaya ya Karagwe, Julius Laiser ameagiza kuondoka wananchi wanaofanya shughuli za kibinadam katika chanzo cha maji mradi wa Kibwela.
Akiweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Kibwela, ambao umevamiwa na wanachi wanaoendesha shughuli za kilimo, Mkuu huyo wa wilaya, alisema serikali imekuwa ikiwekeza fedha nyingi katika miradi ya maji kwa ajili ya wananchi, lakini wananchi wenyewe ndio chanzo kikubwa cha kuharibu miundombinu na kusababisha maji kukauka.
” Moja ya changamoto kubwa katika miaka iliyopita ni upatikanaji wa maji safi na salama , serikali iliunda chombo cha kusimamia miradi ya maji vijijini (RUWASA), lakini niseme tu sisi wenyewe tunaharibu.
“Mimi kama mwakilishi wa serikali sitakubali hujuma au uharibifu wa kazi iliyosimamiwa vizuri, lazima wananchi waheshimu sheria na wachukulie miradi hii kama miradi yao na vizazi vijavyo,”alisema Laizer.
Ametoa wito kwa mamlaka zinazosimamia miradi ya maji wilayani Karagwe kuhakikisha miradi ya maji inapokamilika panakuwepo na maeneo ya kunyweshea mifugo, ili kuhakikisha wafugaji hawatumii maeneo ya vyanzo vya maji kunyweshea mifugo yao.
Kaimu Meneja wa RUWASA, Justo Mutabuzi amesema mradi huo umepunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi na kuifanya Wilaya ya Karagwe kufikia asilimia 74 ya upatinaji wa maji safi na salama.