DC Kigoma ashauri sheria ya kazi iangaliwe upya

MKUU wa wilaya ya Kigoma, Ester Mahawe

MKUU wa wilaya ya Kigoma Ester Mahawe ameshauri bunge kuifumua sheria ya ajira na kuiunda upya kwa madai imekuwa kikwazo katika ufanisi kutokana na baadhi ya watendaji kufanya kazi kwa mazoea.

Mahawe alitoa kauli hiyo wakati akijibu baadhi ya hoja za wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kwenye mkutano ulioongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Abdulrahman Kinana uliofanyika ukumbi wa Kanisa Anglikana mjini Kigoma.

Kauli yake ilitokana na maswali mengi ya wananchi waliohoji namna gani Serikali inawasaidia kupunguza urasimu katika biashara zao na kudai kuwa baadhi ya vipengere vya sheria havina tija lakini wanaishia kusumbuliwa bila sababu.

Advertisement

Alisema watendaji wengi wa serikali hawafanyi kazi kwa vile ni waajiriwa wa kudumu, hivyo ni wakati wa kubadili utaratibu wa ajira ili uwe wa mikataba hata ya miezi mitatu mitatu na baada ya muda huo mfanyakazi afanyiwe tathmini ya utendaji kazi kabla ya kupewa mkataba mpya.

“Bunge lipo kwa ajili ya kubadilisha sheria,hii sheria ya ajira ibadilishwe iwe ya mkataba, kwani itasaidia watu kujituma na kuacha kufanya kazi kwa mazoea, lakini ni wakati wa kuangalia watumishi wa muda mrefu wahamishwe ili kuleta tija,” alisema Mahawe.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo, baadhi ya watumishi wasio waaminifu ndiyo chanzo cha kutengeneza migogoro ya ardhi akisema wengine walifanya hivyo kwa kushirikiana na viongozi wa upinzani waliopita huku akipendekeza waliosababisha migogoro warudishwe Kigoma ili waitatue na ikibidi wachukuliwe hatua za kisheri.

“Kuna kesi mume kauza nyumba akiwa baa mke na watoto wakiwa ndani, hii hata ukikesha hutoweza kuitatua, ilishafika mpaka mahakamani mnunuzi akashinda na zipo nyingi, nyingine mtu anaumwa ardhi yake imechukuliwa, kaenda mahakamani mara mbili anashinda, nilishamwelekeza Mkurugenzi na wanasheria cha kufanya mpaka leo hawajashughulikia, busara itumike kukaa na uyu mzee afidiwe,” alisema.

Katika hatua nyingine Mahawe alisema wakuu wa Idara ni changamoto kwani wanaumiza wateuliwa kwa kuwakwamisha kwenye mambo mengi hivyo akashauri kwamba Mkurugenzi anapotumbuliwa aondoke na wakuu wote wa idara.

Kuhusu tozo kwenye biashara alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), TPA, TASAC , EWURA nao ni shida kwa biashara za mipakani na kikwazo cha maisha ya watu kwa kuwa Wafanyabiashara wanaonunua na kuuza bidhaa katika nchi jirani za Burundi na Congo wanakutana na urasimu kutoka kwenye mamlaka hizo.

Alipendekeza waajiriwa wa Mamlaka za serikali waajiriwe kwa ujuzi (knowledge) wa biashara sio kuangalia ufaulu wa halafu ghafla anapewa ajira ya mshahara mzuri, gari lenye kiyoyonzi, watoto wanasoma shule nzuri jambo alilosema kunakosekana mbinu ya kuishauri serikali badala yake wanabaki kuumiza wananchi.

Aliomba suala la visa ya DRC iondolewe, kwa kuwa Tanzania inapoteza fedha nyingi kwa kigenzo cha ulinzi na usalama, wakati kuna majeshi, wakuu wa mikoa makanali na kuna vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vitafanya kazi ya kulinda mipaka ili biashara zifanyike kihalali nchi ipate pesa.

Nae, Makamu Mwenyekiti wa CCM Abdulrahman Kinana akizungumza alisema kuna vikwazo vingi ambavyo vinapelekea watu kukwama na kukosa maendeleo na kulitaka bunge kufanya marekebisho ya sheria.

Kinana alikumbushia pia kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati akiwaapisha Mawaziri April mwaka huu ambapo aliwaagiza kupitia sheria zote ambazo ni kero kwa wananchi ili wampelekee nay eye atakuwa tayari kuzifuta.

Alisema wakati wowote atakutana na Mawaziri ili awaulize agizo la Rais wamefikia wapi kwani anachojua ni kuwa kiongozi wan chi hataki kuona kunakuwepo na sheria kandamizi kwa anaowaongoza.