DC kuchunguza mikataba ya ajira MDF Mafinga

DC kuchunguza mikataba ya ajira MDF Mafinga

KIONGOZI wa mbio za mwenge wa Uhuru, Abdallah Shaib Kaim amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Linda Salekwa kupitia upya mikataba baina ya muajiri na wafanyakazi wa kiwanda cha Lush Chanzo Wood Industries Ltd cha mjini Mafinga, kinachojishughulisha na utengenezaji wa mbao ngumu (MDF), ili kulinda maslahi ya pande hizo mbili.

Ametoa agizo hilo baada ya Mwenge wa Uhuru kuzindua kiwanda hicho cha kwanza nchini kuanza kuzalisha bidhaa hiyo, inayotokana na mabaki yatokanayo na uchakatwaji wa mazao ya misitu kwa ajili ya kutengenezea samani zenye muonekano wa kuvutia katika soko la ndani na nje ya nchi.

Kiwanda hicho kilichopo katika eneo la Rungemba mjini Mafinga, kimeanzishwa na muwekezaji Zangh Zi Jun kutoka China na kinagharimu dola za kimarekani Milioni 15 ambazo ni sawa na zaidi ya Sh Bilioni 34.

Advertisement

8.

Pamoja na kuweka jiwe la msingi na kupongeza jitihada kubwa zilizofanywa na muwekezaji huyo, kiongozi wa mbio za mwenge alisema; “Uwekezaji huu umetoa fursa ya ajira na unatarajia kuongeza pato la mtu mmoja mmoja, halmashauri ya mji Mafinga, Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa na taifa kwa ujumla.”

Kwa kujali maslahi ya wafanyakazi aliitaka wilaya hiyo kupitia ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuunda timu kazi itakayoichambua upya mikataba ya wafanyakazi, ili kuona kama haki zao ikiwemo mishahara yao na marupurupu mengine yanazingatiwa.

 Aidha alikitaka kiwanda hicho kuzingatia sheria mbalimbali za uanzishwaji wake, ikiwa ni pamoja na kuwalinda wafanyakazi wake wakati wote wawapo kazini.

Awali akitoa taarifa ya uwekezaji huo mkubwa Meneja Msaidizi wa Kiwanda hicho, Justine Mligo alisema mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa itakayosaidia kutunza na kuhifadhi mazingira kwa kupunguza uchafu, kwani malighafi inayotumika ni mabaki yatokanayo na uchakatwaji wa mazao ya misitu.

Naye Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi amemshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji hatua inayowavutia wawekezaji wa ndani na nje kutumia fursa zilizopo kuwekeza.

Chumi alisema kiwanda hicho kitaleta neema kubwa jimboni mwake, kwani kinatarajia kutoa fursa ya ajira za muda mfupi na muda muda mrefu na kuharakisha ukuaji wa uchumi wa watu na Taifa.

“Niwaombe sana kwa kuwa bidhaa inazalishwa Mafinga Tanzania, basi muweke nembo itakayotambulisha bidhaa hiyo katika soko la kimataifa kwamba inatoka Tanzania ili kuitangaza nchi yetu,” alisema.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *