DC Lushoto atangaza kampeni ya utalii

MKUU wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, Japhari Kubecha ametangaza kuanza kampeni ya kutangaza utalii uliopo wilayani humo.

Akizungumza na HabariLEO, mapema leo, DC Kubecha amesema Watanzania wanadhani Lushoto ni sehemu ya kilimo tu, lakini kuna maeneo ya kimkakati ya utalii.

“Mimi na timu yangu, kupitia kamati ya usalama ya wilaya na maofisa wa utalii Halmashauri ya Lushoto na Bumbuli tumejipanga na tumeunda timu ya kuanza kutangaza vivutio,” amesema DC Kubecha.

DC Kubecha amesema kampeni hiyo ni kuelekea katika tamasha lao lijulikanalo kama Lushoto Utalii Festival ambalo litafanyika mwezi Julai, 2024.

“Tunataka tuoneshe umma wa Watanzania pamoja na dunia kwamba Lushoto ina vivutio vingi,” ameongeza DC Kubecha.

Akitaja vivutio vilivyomo wilayani humo, DC Kubecha amesema kuna maporomoko ya maji yapatayo matano, lakini misitu ya asili mikubwa sio chini ya 10 na vivutio vingine ikiwemo mali kale.

Amewataka Watanzania kutembelea wilaya hiyo kujionea namna Lushoto ilivyo na vivutio vya utalii.

Habari Zifananazo

Back to top button