DC Manyoni kushughulikia malalamiko mbolea ya ruzuku

DC Manyoni kushughulikia malalamiko mbolea ya ruzuku

MKUU wa Wilaya ya Manyoni, Kemilembe Lwota, ametaka dhana ya hakuna aliye juu ya sheria izingatiwe na ameahidi kushughulikia malalamiko ya madiwani dhidi ya wakala wa mbolea ya ruzuku kwa kuwa inaashiria kuwepo hujuma.

Ametoa ahadi hiyo kwenye kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani leo Februari 23, 2023 baada ya malalamiko ya madiwani kuhusu wakala wa mbolea ya ruzuku.

Diwani wa Mkwese, Robert Chanzi, amesema wakala huyo ananyima wakulima mbolea, hata walioongozana na mtumishi wa serikali anayesimamia mpango huo, wote waliishia kukamatwa na polisi, kuwekwa mahabusu kwa maelekezo ya wakala huyo.

Advertisement

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Alexander Mpombwe,  amesema hana majibu ya hoja hiyo, licha ya kuwasiliana naye ili yeye au mwakilishi wake ahudhurie kikao hicho, lakini hawakuhudhuria.

DIWANI wa Kata ya Manyoni “B”, Mapunda Simon, akizungumza kwenye kikao hicho. (Picha zote na Editha Majura).

Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Ahmed Makelle, amekana kufahamu lolote kuhusu malalamiko  hayo, huku mwanasheria wa halmashauri hiyo akishindwa kujibu lolote kwa kuwa hakuwa na maelezo yanayojitosheleza kisheria kumuweka kwenye nafasi nzuri ya kulizungumzia.

Diwani wa Kata ya Nkonko, Ezekiel Samuel Ezekiel, amesema mzunguko katika kusemea suala hilo unaashiria kuwepo sintofahamu katika utekelezaji wa mpango huo, ni dhahiri inatakiwa nguvu ya ziada kulishughulikia.

Naye Diwani wa Manyoni “B”, Mapunda Simon, amesema kumbukumbu zake zinaonesha wakala huyo alipokea tani 140 za mbolea ya ruzuku, lakini mifuko 400 ilipelekwa Tabora huku wengi wa wananchi walioandikishwa ili wanufaike na mbolea hiyo wilayani Manyoni wakiwa hawanufaiki.

Mjadala wa hoja hiyo umehitimishwa kwa DC Kemilembe kutoa ahadi hiyo akisema kwa jinsi mjadala ulivyokwenda, amejiridhisha kuwa suala hilo linatakiwa kufuatiliwa kwa kina na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria, kwa sababu hakuna aliye juu ya sheria.

MWENYEKITI wa Baraza la Madiwani Halmashauri ya Manyoni, Jumanne Nlagaza, akifungua kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani leo.
/* */