DC Mbogwe awataka wanawake kushiriki maendeleo

GEITA: Wanawake wametakiwa kuendelea kujituma na kushiriki kwenye shughuli za maendeleo ili kujiinua kiuchumi na kujiletea maendeleo katika familia.

Pia wametakiwa kutovumilia vipigo kwenye ndoa kwa kuwa hata maandiko hayajasema mwanamke akae ndani anyanyasike na kupigwa tu.

Hayo yamesemwa leo Machi 8, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Sakina Mohamed katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Dunia kwa Mbogwe yanafanyika kata ya Bukandwe.

Advertisement

“Ukiona ndoa ni vipigo, sepaa, lakini pia jisimamieni kiuchumi, ukiwa na uchumi wako hautatetereka, fanyeni kazi kwa bidii kwa ajili ya maendeleo yenu binafsi na familia zenu, ” amesema Sakina.

Kauli ya Sakina imekuja baada ya kupokea ripoti ya takwimu ya mwaka 2022/2023 inaonyesha wanawake waliofanyiwa ukatili ni zaidi ya 1, 309 kwa taarifa zilizoripotiwa Polisi vile vile ukatili wa kihisia ni zaidi ya 2,100.

Aidha, amewahimiza wana Mbogwe kuzingatia kauli mbiu ya siku ya Wanawake duniani inayosema “Wekeza kwa Wanawake ili kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii” na kudai kuwa kauli mbiu hiyo inaonesha ni kwa umuhimu wa pekee jamii inapaswa kuthamini na kutambua nafasi ya wanawake.