DC Msando: Hakuna mwandishi atakayenyanyaswa

DC Msando: Hakuna mwandishi atakayenyanyaswa

MKUU wa Wilaya ya Morogoro,  Albert Msando amewataka waandishi wa habari, kufanya kazi zao kwa kufuata sheria, taratibu na weledi na kwamba hakuna atakayenyanyaswa, wala kunyang’anywa vitendea kazi, wakati wa utekelezaji wa majukumu yake wilayan humo.

Msando alisema hayo katika mdahalo ulioandaliwa na Chama cha Klabu ya Waandishi  wa Habari Mkoa wa Morogoro (Moro PC), uliokuwa na  dhima ya kulinda usalama wa mwandishi wa habari akiwa kazini, uliodhaminiwa na  Shirika la Kimataifa la Kusaidia Vyombo vya Habari (IMS) na kusimamiwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini (UTPC).

Alisema kuwa waandishi wa habari watalindwa na kuwezeshwa kufanya kazi zao kwa ufasaha na kuendelezwa kiuchumi, ili waweze kuendana na hali halisi ya kimaisha.

Advertisement

Msando pia aliziagiza taasisi za serikali zilizopo wilayani humo, kuacha urasimu wa utoaji habari kwa waandishi wa habari, kwa kuwa wapo kwa mujibu wa katiba na mikataba ya kimataifa katika kutekeleza majukumu yao.

Naye Mwenyekiti wa Moro PC , Nickson Mkilanya akimkaribisha Mkuu wa Wilaya katika mdahalo huo, aliziomba  mamlaka za serikali mkoani Morogoro, kuwalinda na kuwapatia ushirikiano waandishi wa habari,  ili kuweza kuhabarisha umma, kwa kuwa hiyo ni haki ya kikatiba.

Nao baadhii ya waandishi wa habari waandamizi,  Idda Mushi na Aziz Msuya wakizungumza kwa nyakati tofauti, walisema kuna haja ya vyombo vya ulinzi na usalama kuwalinda waandishi wa habari, kwa vile  wanasaidia kusukuma maendeleo ya Taifa.

Pia walitumia mdahalo huo kutoa rai kwa wanataaluma wenzao, kutoutumia uhuru wa habari vibaya,  bali wafuate sheria  na  kuzingatia taratibu na maadili ya uandishi wa habari.