DC Mtwara aagiza wananchi walipwe fidia

DC Mtwara aagiza wananchi walipwe fidia

MKUU wa Wilaya ya Mtwara, Dustan Kyobya, amemtaka Mkurungezi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, mkoani humo kuhakikisha wananchi waliotoa eneo la uwekezaji la Mtepwezi Kata ya Likombe wanalipwa fidia yao yote ifikapo Desemba mwaka huu, mara baada ya kumaliza kuhuisha uthamini wa eneo hilo.

Ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi ambao walitoa eneo hilo katika mkutano ambao uliofanyika leo eneo la Mtepwezi.

“Mkurungezi kama ulivyoahidi hakikisha unalipa fidia, lakini baada ya kufanya uthamini upya kwa mujibu wa sheria, ili kuhuisha uthamini, uthamini wa wakati ule (2016) kwa mujibu wa sheria umepitwa na wakati, ahuishe uthamini ili uendane na uthamini wa sasa,” amesema.

Advertisement

Eneo hilo lilifanyiwa uthamini mwaka 2016, baada ya kuchukuliwa na kutengwa na serikali katika manispaa hiyo kwa ajili ya uwekezaji.

“Lakini kabla ya kulipa tunaanza uhakiki wa mipaka, kupima na kujua kila mtu katika eneo lake baada ya hapo kufanya uthamini wa kila mtu na mali zake katika eneo husika na mwisho wa siku kulipa fidia,” amesema.

DC huyo amemtaka Kamishna wa Ardhi kushirikiana na ofisi ya mkurungezi huyo kupima maeneo hayo kwa kutumia vifaa vya GPS. Kyobya amesema hatua hiyo itasaidia pia kuondoa sintofahamu kwa wamiliki wa eneo, ambapo kumekuwepo na mgogoro.

“Wapo wananchi wanasema hawajalipwa, wengine wanasema kuwa wameonewa hali ambayo imenisukuma kutoa maagizo ili kumaliza mgogoro katika eneo hilo ambalo limetengwa kwa ajili ya uwekezaji,” amesema.

Kyobya amesema sehemu ya eneo Hilo limeshalipiwa na mwekezaji wa Alistair Group, ambaye ameshaingia mkataba na serikali na taratibu zingine zinaendelea.