SHIRIKA la Umeme nchini (TANESCO) Mkoa wa Mwanza limeshauriwa kuwa na mkakati endelevu wa zoezi la upandaji miti.
Ushauri huo umetolewa leo Machi 7, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi wakati wa zoezi la upandaji miti la kusherehekea siku ya Wanawake Duniani. DC Mwakilagi ameipongeza Tanesco mkoani hapa kwa kupanda miti 120 ya matunda na vivuli katika zahanati ya Mahina.
‘’Naipongeza sana Tanesco Mwanza kwa kuja na zoezi hili upandaji miti. Nawaomba sana Tanesco zoezi hili liwe endelevu na ikiwezekana liwe linafanyika wiki kwa wiki’’ amesema Makilagi.
Amesema atafuatlia eneo maalumu katika wilaya yake ili tanesco itengewe kwajili ya kuweza kupanda miti.
Ametaka taasisi na mashirika mbalimbali mkoani Mwanza kuja na mpango maalumu wa upandaji miti kama wa shirika hilo.
Amesema takribani miaka mitatu kumekuwa na ukosefu wa mvua hivyo zoezi la upandaji miti litasaidia sana katika kuweza kuleta mvua. Ofisa Masoko wa Tanesco Mwanza, Joyce William amesema shirika lao litakuwa na mipango endelevu ya kupanda miti kwa kuwa miti imekuwa ikileta mvua.
Amesema Shirika lao ni watumiaji wakubwa sana wa miti. Amesema inaponyesha mvua inasaidia sana upatikanaji wa maji ambapo maji hayo hutumika katika uzalishaji wa umeme.