DC Rungwe azindua vyumba vya madarasa

MKUU wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Haniu amezindua vyumba  sita vya madarasa katika shule ya Msingi Kinyangwa iliyopo Kijiji cha Katunduru Kata ya Ilima.

Mradi wa ujenzi wa vyumba hivyo umetekelezwa na Kampuni ya Bioland kupitia mradi wa Cocoa for School kwa gharama ya Sh million 64, huku wananchi wakichangia nguvu zao kwa zaidi ya Sh milion 30.

Kampuni ya Bioland hujishughulisha na ununuzi wa zao la kakao na faida yake huirejesha kwa jamii Kwa  ajili ya miradi ya maendeleo.

Akizundua madarasa hayo Haniu ameishukuru kampuni hiyo kwa kazi kubwa waliyoifanya na kwa kufanya hivyo itaongeza ufaulu katika shule hiyo, baada ya mazingira ya kusomea na kujifunza kuboreshwa.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuboresha mazingira mazuri ya kufundishia, hivyo wadau mbalimbali pamoja na wananchi hawana budi kumuunga mkono sambamba kutunza miundombinu ya elimu, ili ikinufaishe kizazi hiki na kijacho.

Haniu ameagiza wazazi wote katika kijiji hicho kujitokeza na kuchangia chakula cha mchana shuleni,  ikiwa ni nyenzo imara ya kuongeza ufaulu sanjari na kuondoa udumavu na utapiamlo kwa watoto.

Wakati huohuo Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Renatus Mchau ameeleza kuwa ufaulu kwa wanafunzi wa elimu ya Msingi umeendelea kupanda mwaka hadi mwaka kwa asilimia 93.7 na hii imechangia na ufundishaji mzuri wa walimu, ubora wa miundombinu ya kufundishia na chakula shuleni.

Mchau ameonya baadhi ya walimu kutumia muda wao vibaya, badala ya kufundisha wanafunzi na hivyo kusababisha wanafunzi kukosa maarifa na ujuzi hatimaye kushindwa mitihani yao ya mwisho.

Katika hatua nyingine uongozi wa Kampuni ya Cocoa for School, umeeleza kuwa utaendelea kuisaidia shule hiyo kwa kukarabati ofisi ya walimu pamoja na vyumba vingine vitatu  vya madarasa vilivyobaki.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button