DCEA: Vijana acheni kilimo cha bangi
MANYARA: Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini (DCEA) imewataka vijana kuachana na biashara, kilimo na matumizi ya bangi katika kujiongezea kipato badala yake kulima kilimo mbadala.
Imeelezwa kuwa vijana wana fursa ya kulima mazao mbadala ya mahindi,maharage na alizeti na kujiongezea kipato badala ya kukimbilia kulima bangi Kwa kuwa inapoteza nguvu kazi ya taifa na kuharibu vyanzo vya maji.
Kamshina Jenerali wa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya Aretas Lyimo akiongea na Waandishi wa habari wilayani Babati mkoani Manyara amesema kuwa Ili kukuza uchumi endelevu ni muhimu kukomesha matumizi ya dawa za kulevya nchini.
Wazazi, viongozi wa dini, serikali na jamii wanawajibu wa kwanza wa kukemea matumizi ya dawa hizo kwa kuwa wanaotumia ni watoto,vijana, wanafunzi hivyo ni muhimu kutambua na kufuatilia mienendo yao.
Operesheni endelevu itafanyika katika Mikoa iliyokithiri kwa kilimo hicho na Wilaya zenye matumizi ya Bangi Ili kubaini ukubwa wa tatizo..
Ameeleza kuwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan amezungumzia kukithiri kwa matumizi ya Bangi nchini hivyo Mamlaka hiyo inafanya jitihada ya kuyamaliza.
Ametaja kuwa katika operesheni iliyofanyika mwaka 2023 watu (19) wamekamatwa Mkoa wa Arusha, (11) Kilimanjaro, (19) Morogoro, Iringa (9) na Mara (11) wakijihusisha na biashara,kilimo na matumizi ya Bangi.