DCEA yakamata dawa za kulevya kilo 3,182

DAR ES SALAAM: MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya Tanzania (DCEA) imekatama jumla ya Kilogramu 3,182 za dawa za kulevya aina ya Heroin na Methamphemine zikiwa kwenye vifungashio vya kahawa na majani ya chai.

Dawa hizo zimekamatwa katika operesheni maalum iliyofanyika jijini Dar es Salaam na Iringa kati ya Desemba 5 hadi 23, 2023.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Desemba 27, 2023 Kamishna Jenerali, Aretas Lyimo amesema, tangu udhibiti uanze DCEA hazijawahi kukamata kiasi kikubwa cha dawa  kama ilivyo sasa na iwapo zingefanikiwa kuingia sokoni watu milioni 76.3 wangeathirika.

“Ukamataji huu umeokoa nguvu kazi yaani Tanzania tupo idadi ya watu milioni 60 hizi dawa zingefanikiwa kuingia sokoni basi zingeathiri si tu wanzania bali hata mataifa mengine maana nyingine zilikuwa zikisafirishwa nchi nyingine,”amesema Lyimo.

Akifafanua Lyimo amesema, kiasi hicho cha dawa kinajumuisha kilogramu 2, 180.29 za dawa aina ya Methamphemine na kilogramu 1001.71 aina ya Heroin zilizokamatwa katika wilaya za Kigamboni, Ubungo na Kinondoni kwa jijini Dar es Salaam na mkoani Iringa.

Amesema, katika operesheni hiyo  watu saba wamekamatwa  kati yao wawili ni raia kutoka bara la Asia.

Aidha, Lyimo amesema mbinu ambayo imekuwa ikitumika kufunga dawa hizo kwenye vifungashio vya bidhaa zenye chapa mbali mbali ikiwemo kahawa na majani ya chai inatumika kwa lengo la kurahisha usafirishaji wake na kukwepa kubainika.

Amesema dawa ya Methamphemine ni dawa mpya ya kulevya iliyopo katika kundi la vichangamshi saw ana cocaine.

“Dawa hii huwa kwenye mfumo wa vidonge, unga au chembechembe mithili ya chumvi ang’avu yenye rangi mbali mbali ambayo huzalishwa kwenye maabara bubu kwa kuchanganya aina mbali mbali za kemikali bashirifu,”amesema Lyimo.

Lyimo amesema Mamlaka inatoa onyo kwa wote wanaoendelea kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya hapa nchini kuacha badala yake wajikite kwenye biashara nyingine halali kwani DCEA imejidhatiti kukomesha biashara ya dawa ya kulevya nchini.

“Mamlaka inaishukuru serikali ya  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha mamlaka katika kutekeleza kazi zake kwa ufanisi mkubwa,”amesema Lyimo.

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button