Deni la mahari sh 500,000 sababu ya Mkwe kuuawa
MOROGORO: Watu wanne wa familia moja akiwemo Masele Machibya Masele (65) mkulima na mkazi wa Tabora wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kula njama na kumuua Hassan Ngema (51) mkulima na mkazi wa Kijiji cha Itegete, wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro ambaye alikuwa anadaiwa kushindwa kulipa deni la mahari ya Sh 500,000.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo , Alex Mkama amesema hayo jana mjini Morogoro kuwa tukio hilo lilitokea mwishoni mwa Agosti mwaka huu katika kijiji hicho kilichopo wilayani Kilombero.
Mkama amewataja watuhumiwa waliokamatwa ni Masele Machibya Masele (65), mkulima na mkazi wa Tabora ,Mwalu Ndama Hassan (18), Pawa Ndama Kema (16) na Rehema Masele (35) ,wote ni wakulima na wakazi wa kijiji hicho.
Amesema watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaiwa walikula njama ya kumuua Hassan Ngema (51) mkulima na mkazi wa Itegete , ambapo kimsingi inadaiwa alikuwa ameshindwa kulipa deni la mahari.
“Hawa ni wafamilia moja , Masele Machibya Masele ni Baba mkwe wa marehemu , alitoka Tabora kuja kumdai mahari mkwewe , na hao wengine ni mke na watoto wa marehemu “ alisema Mkama
“Sasa walipoona huyo ( Marehemu ) amekuwa mkaidi muda mrefu halipi mahari na ameshapata watoto tayari waliamua kula njama na kumuua “ amebainisha Kamanda Mkama
Amesema baada ya kutokea kwa mauaji hayo watuhumiwa wamekamatwa upekelezi unaendelea na utakapokamilika watafikishwa Mahakamani.
Kwa mujibu Kamanda wa Polisi wa mkoa huyo kuwa,mahari hiyo iliyokuwa inadaiwa ni ya muda mrefu ukizingatia ( Marehemu) alishakuwa na mtoto mwenye kufikisha umri wa miaka 16 ,na alibakiza kiasi cha Sh 500,000.
“Hizi ndizo fedha alikuwa anadaiwa kuzilipa na alikuwa akizungusha kipindi chote hicho , hivyo baba mkwe ametoka Tabora kuja (Kilombero – Morogoro) kufuata mahari iliyobakia” amesema Mkama
Ameongeza kuwa kabla ya kifo cha marehemu , Baba mkwe huyo alikaa nyumbani kwa marehemu kwa muda wa siku tatu akiwa nafuatilia hiyo mahari na kwamba siku ya nne (maheremu) alipotea katika mazingira ambayo yalikuwa na utata.
Kamanda wa Polisi wa mkoa amesema ,baada ya kupotea kwa marehemu huyo, wasamaria wema walitoa taarifa Polisi na ufuatiliaji ulianza mara na hatimaye ikagundulika kuwa ameuawa .
“Kwa sasa tumeikamata hii familia na kwamba upelelezi unaendelea na ukikamilishwa watuhumiwa watafikishwa kwenye vyombo vya sheria “amesema Kamanda Mkama.