Deni la Taifa bado himilivu – Mwigulu

DENI  la Serikali hadi Aprili 2023, lilikuwa shilingi trilioni 79.10, sawa na ongezeko la asilimia 13.9 ikilinganishwa na shilingi trilioni 69.44 Aprili 2022.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba akiwasilisha makadirio ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Bungeni mjini Dodoma leo Juni 15, 2023.

Amesema kati ya kiasi hicho, deni la ndani ni shilingi trilioni 27.94, sawa na asilimia 35.3 na deni la nje ni shilingi trilioni 51.16, sawa na asilimia 64.7.

“Kati ya deni la nje, deni lenye masharti nafuu ni shilingi trilioni 37.69, sawa na asilimia 73.6, hivyo, sehemu kubwa ya deni la nje ni mikopo yenye masharti nafuu,”amesema.

Amesema, tathmini ya uhimilivu wa deni la Serikali iliyofanyika Desemba 2022 ilionesha kuwa deni la Serikali ni himilivu katika kipindi cha muda wa kati na mrefu.

Mwigulu amesema kuwa matokeo ya tathmini yanaonesha uwiano wa thamani ya sasa ya deni la Serikali kwa Pato la Taifa ni asilimia 32.5 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55; uwiano wa thamani ya sasa ya deni la nje kwa Pato la Taifa ni asilimia 18.1 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40.

Aidha, uwiano wa thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 120 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 180.

Amesema, uwiano wa ulipaji wa deni la nje kwa 60 mauzo ya bidhaa na huduma nje ni asilimia 13.5 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 15.

“Matokeo haya yanawiana na matokeo ya tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanywa na Shirika la Fedha la Kimataifa na kuchapishwa Aprili 2023,”amesema.

Amesema, katika kuhakikisha kuwa Deni la Serikali linaendelea kuwa himilivu, Serikali inatekeleza hatua mbalimbali ikiwemo kuhakikisha mikopo inayopewa kipaumbele ni ile yenye masharti nafuu kadri inavyopatikana.

Hali hiyo inajidhihirisha katika bajeti inayopendekezwa ambapo mikopo nafuu imeongezeka kwa asilimia 22.8 na yenye masharti ya kibiashara imepungua kwa asilimia 14.4.

“Kuelekeza mikopo yenye masharti ya kibiashara katika miradi inayochochea kasi ya ukuaji wa uchumi na mauzo nje ya nchi, kuboresha mikakati ya kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ili kuhakikisha sehemu kubwa ya bajeti inagharamiwa na mapato ya ndani pamoja na kupunguza matumizi yanayoweza kuepukika bila kuathiri uendeshaji wa shughuli za Serikali.”Amesema

Habari Zifananazo

Back to top button