MATAIFA ya Denmark na Rwanda yamechapisha taarifa ya pamoja mjini Copenhagen yakiahidi kuimarisha ushirikiano wa karibu ikiwemo mpango wa kuwapeleka nchini Rwanda waomba hifadhi wanaowasili Denmark.
Taarifa hiyo imesema nchi hizo mbili zinafanyia kazi uwezekano wa kuwa na mpango huo ambapo waomba hifadhi nchini Denmark watasafirishwa hadi Rwanda wakisubiri maombi yao kufanyiwa kazi.
Taarifa hiyo ya pamoja imesema makubaliano yoyote yatakayofikiwa yatazingatia wajibu wa kimataifa wa nchi hizo juu ya kuwalinda wakimbizi na kuheshimu haki za binadamu.
Rwanda tayari ilikwishafikia makubaliano ya aina hiyo na Uingereza, lakini utekelezaji wake unakabiliwa na vizingiti vikiwemo vya mahakamani.
Wengi wanaoukosoa mpango huo wanasema unakiuka utu na haki za waomba hifadhi na mashirika kadhaa ya haki za wakimbizi yamefungua kesi nchini Uingereza kuupinga.