Dhana ya ‘mtoto ni wa jamii’ suluhu ukatili dhidi yao

NOVEMBA 25 mwaka huu, Tanzania iliungana na wanaharakati wengine duniani kuanza kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto ambapo kilele chake kilikuwa juzi Desemba 10, Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu.

Wanaharakati wa haki za wanawake kila tarehe 25 Novemba huadhimisha siku ya kupinga ukatili wa kijinsia tangu mwaka 1981.

Tarehe hiyo ilichaguliwa kuwaenzi wanawake wa Mirabal sisters, wanaharakati watatu wa kisiasa kutoka Jamhuri ya Dominika waliouawa kikatili mwaka 1960 kwa amri ya mtawala wa nchi hiyo, Rafael Trujillo (1930-1961). Desemba 20, 1993, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio la Kutokomeza Ukatili kwa Wanawake kupitia azimio namba 48/104, kuweka njia kuelekea kutokomeza ukatili huo duniani.

Hatimaye, Februari 7, 2000, UN ilipitisha azimio namba 54/134, likiitaja rasmi Novemba 25 kuwa Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukatili kwa Wanawake.

Siku hiyo hushirikisha serikali, mashirika ya kimataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) kwa pamoja huandaa shughuli za kuongeza uelewa kwa umma juu ya suala hilo kila mwaka.

Pamoja na Tanzania kuendesha kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto kila mwaka, bado vitendo vya ukatili dhidi ya makundi hayo vimeendelea kuripotiwa nchini.

Takwimu za Jeshi la Polisi Tanzania katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2021 zinaonesha matukio 11,499 ya ukatili kwa watoto yalitolewa taarifa katika vituo vya polisi. Mikoa iliyoongoza ilikuwa ni Arusha (808), Tanga (691), Shinyanga (505), Mwanza (500) na Mkoa wa Kipolisi Ilala (489).

Aidha, makosa yaliyoongoza kwa idadi kubwa ni ubakaji (5,899), mimba kwa wanafunzi (1,677) na ulawiti (1,114). Juni 6 mwaka huu, akiwa Dodoma katika Shule ya Msingi Mnadani alipokuwa akizungumza na wanafunzi na walimu wa shule hiyo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima, aliwataka watoto kote nchini kufichua viashiria vya vitendo vya kikatili dhidi yao vinavyotokea hasa katika maeneo ya shule na nyumbani.

Dk Gwajima aliwasisitiza watoto hao kutokuogopa na badala yake waonapo vitendo vya ukatili au viashiria watoe taarifa kwa watu wanaowaamini ikiwepo dawati la jinsia katika vituo vya polisi.

Alisema serikali kupitia wizara hiyo yenye dhamana na watoto iliandaa Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 ambayo imeainisha haki tano (5) za msingi za mtoto ikiwepo ya Kuishi, Kulindwa, Kuendelezwa, Kushiriki na haki ya Kutobaguliwa na kuratibu utungwaji wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009.

Aidha, Dk Gwajima alisisitiza mapambano dhidi ya ukatili kwa watoto akiwa Dar es Salaam Novemba 25 wakati akizindua maadhimisho ya kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

Alisema vitendo vya ukatili wa vipigo na kingono vinapaswa kupingwa na jamii ivunje ukimya na kuzungumza lugha zenye uwazi na kuwaelewesha watoto vitendo vya ukatili vinafanyikaje na namna ya kutoa taarifa.

Wakati hayo yakijiri, mkoani Mbeya nako kumekuwa kukiripotiwa matukio ya mara kwa mara ya ukatili dhidi ya watoto ikiwemo ubakaji na ulawiti, mimba kwa wanafunzi, ukatili majumbani na kuuawa.

Matukio haya yanausukuma mkoa huo kupitia Jeshi la Polisi, Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto kwa kushirikiana na wadau kuendesha kampeni za utoaji elimu kwa makundi mbalimbali kukabiliana na ukatili dhidi ya watoto mkoani Mbeya.

Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto mkoani Mbeya, Loveness Mtemi anasema kati ya kesi zinazoripotiwa kwenye ofisi yake kuhusu ukatili dhidi ya watoto, nyingi zinahusisha vitendo vya ukatili wa kingono na vipigo na vimewaathiri watoto kiafya, kiakili na kielimu.

“Watoto wamekuwa wakipigwa, mzazi haoni shida kumchoma moto mtoto kwa sababu tu alikosa, ilitokea mtoto mmoja amechukua yai amechemsha amekula, inawezekana alikua na njaa lakini mama alipofika alimchoma moto vidole,” anasema Mtemi.

Anasema malezi yana nafasi kubwa kufanya vitendo vya ukatili kutokomea na malezi yasiyo bora yamewaathiri sana watoto. Anaonya wazazi kuwa makini na watu wanaowaachia watoto wao na kuwaasa kuacha tabia ya kutumia maneno yasiyofaa wanapozungumza au kuwaonya watoto.

Anasema kitengo hicho kwa kushirikiana na wadau wanatoa elimu shuleni na kwenye mikusanyiko ya wananchi kuhusu ukatili wa kijinsia.

Akitoa elimu kuhusu ukatili kwa watoto kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Sinde na Shule ya Msingi Mlimani za mkoani Mbeya, David Mtulo wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Mbeya, anawaeleza wanafunzi hao aina ya ukatili, namna ya kuripoti vitendo hivyo na madhara huku akiwaasa kuepuka tamaa ambazo husababisha kufanyiwa ukatili na kuzimwa ndoto zao za kielimu.

Kwa upande wake Mwalimu wa malezi katika Shule ya Sekondari Sinde, Tumpe Mwalingo, anasema changamoto wanayokabiliana nayo katika mapambano ya ukatili kwa watoto ni kukosa ushirikiano baina ya wazazi na walimu huku wazazi/ walezi wengi wakiacha jukumu la malezi kwa walimu.

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Sauti ya Mama Afrika mkoani Mbeya ambalo linajihusisha na kupinga ukatili wa wanawake na watoto, Tabitha Bugali, anasema wanashirikiana na serikali na wadau wengine kutoa elimu dhidi ya vitendo vya ukatili kwa watoto kwa kutumia majukwaa ikiwemo shuleni na vyombo vya habari.

“Ili tuweze kukabiliana na tatizo hili ni lazima tuanzie kwenye malezi ya watoto wetu na kila mmoja amwone mtoto wa mwenzie ni wake, mimi nina miaka 65 sasa na katika wakati wetu vitendo hivi havikuwepo sana kwa sababu tulishirikiana suala la malezi ya watoto kama jamii,” anasema Bugali.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, anasema vita ya ukatili wa kijinsia kwa watoto itafanikiwa ikiwa watashirikiana na wadau kupinga ukatili kwa kutoa elimu endelevu dhidi ya vitendo hivyo. Madhara ya ukatili kwa watoto Mwanasaikolojia kutoka Hospitali ya Rufaa Mbeya, Betuna Mwamboneke, anasema: “Watoto wengi wanaofanyiwa ukatili wanapata tatizo la kisaikolojia la wasiwasi linalomfanya mtoto ashindwe kujiamini, kusimama mbele za watu na kuzungumza anakuwa na woga usioelezeka, lakini pia unaweza kumsababishia mtoto kujitenga na kuona watu wote ni wabaya,” alisema Homera.

“Mtoto anakuwa hawezi kufuata sheria, hajali maumivu ya watu wengine sababu naye alishawahi kuumizwa, unakuta ndio hao wanafanya matukio ya hatari mtaani, hawezi kufanya vizuri shuleni au anawafanyia ubaya wengine kwa lengo la kulipiza kisasi na mwingine akipata familia hawezi kuwa na malezi bora kwa watoto wake,” anasema Mwamboneke.

SULUHISHO

Mwamboneke anasema suluhisho la ukatili kwa watoto ni wazazi na walezi kuzingatia malezi bora na jamii kushirikiana kuendelea kutoa elimu juu ya vitendo hivi vya ukatili dhidi ya watoto.

“Lakini tunaweza kuzitumiaje hizi siku 16 za kukabiliana na vitendo hivi, kitu cha kwanza mimi ambacho huwa naamini katika kusuluhisha tatizo lolote ni mtu kuwa na uelewa juu ya hilo tatizo, wanasheria, madaktari na wanasaikolojia wote tutoe elimu,” anasema Mwamboneke.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x