Diaspora wamwaga fedha uwekezaji Tanzania

DODOMA; SERIKALI imesema mwamko wa Diaspora katika kuchangia maendeleo ya Taifa umeendelea kuongezeka.

Kauli hiyo imetolea na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki January Makamba, alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa Mwaka wa fedha 2024/25 bungeni mjini Dodoma leo.

“Kwa kuzingatia umuhimu wa diaspora, wizara imeendelea kushiriki katika kuweka mazingira wezeshi yakiwemo ya kisera na kisheria kama hatua muhimu ya kuchochea ushiriki wa Watanzania waishio nje ya Nchi (Tanzania Citizen Diaspora) na raia wa nchi nyingine wenye asili ya Tanzania (Tanzania Non Citizen Diaspora) katika maendeleo ya Taifa.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/diaspora-kushiriki-maoni-dira-ya-maendeleo-2050/

“Hatua hizi ni pamoja na kujumuisha masuala ya Diaspora katika mapitio ya Sera Mpya ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 na kutoa Hadhi Maalum (Special Status) kwa raia wa nchi nyingine wenye asili ya Tanzania ili kuwapa haki na upendeleo mahsusi.

“Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, mwamko wa Diaspora katika kuchangia maendeleo ya Taifa umeendelea kuongezeka, ambapo wameendelea kuchangia katika sekta mbalimbali zikiwemo nyumba, kilimo, teknolojia, utalii, uchumi wa buluu,afya na elimu.

“Mathalan, katika kipindi cha mwezi Januari hadi Desemba 2023 uwekezaji wa Diaspora katika sekta nyumba na viwanja, kupitia Shirika la Nyumba la Taifa na kampuni za KC Land Development Plan na Orange Tanzania ulifikia shilingi bilioni 9.28 kutoka Sh bilioni 4.4 kwa mwaka 2022.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/diaspora-wawekeza-bil-4-4-nyumba-viwanja/

“Aidha, katika kipindi cha mwezi Januari hadi Desemba 2023 uwekezaji wa diaspora katika Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja (UTT-AMIS) ulikuwa Sh bilioni 6.4 kutoka Sh bilioni 2.5 za kipindi cha mwezi Januari hadi Desemba, 2022. Vilevile, fedha zilizotumwa nchini na Diaspora kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Desemba 2023 zilikuwa Dola za Marekani milioni 751.6,” amesema Waziri Makamba.

Pia amesema Kampuni ya Livy Africa ambayo inamilikiwa na Diaspora imewekeza katika uzalishaji wa chokoleti (Mababu Chocolate) kwa kutumia kakao kutoka Kyela, Mbeya.” Uwekezaji huu umetoa ajira kwa vijana na kuongeza kipato kwa wakulima wa zao la kakao wilayani Kyela na maeneo jirani.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/makamba-aanika-vipaumbele-5-mambo-ya-nje/

“Kampuni hii imeendelea kutoa elimu ya kuongeza thamani ya mazao na bidhaa kwa wakulima wadogo. Vilevile, mwezi Machi 2024 Diaspora kwa kushirikiana na Taasisi ya Al- Wadood ya Oman walitoa misaada ya kijamii ikiwemo uchimbaji wa visima vya maji katika vijiji vilivyoko Wilaya za Wete na Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

“Serikali pia inatambua na kupongeza mchango wa Diaspora katika kuanzisha mfumo wa kifedha wa NALA unaotoa huduma ya kutuma fedha kutoka nchi 21 zilizopo Ulaya na Amerika kwenda nchi za Afrika, ikiwemo Tanzania. Mfumo huu ni kielelezo cha ubunifu wa Diaspora wenye mchango muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu.

“Serikali itaendelea kuwashawishi Diaspora kuchangia zaidi katika maeneo haya na mengine ya kimkakati, ikiwemo rasilimaliwatu, ujuzi na teknolojia hususan akili mnemba (Artificial Intelligence), madini ya kimkakati, uchumi wa buluu na gesi asilia,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button