Diaspora wawekeza bil 4.4/- nyumba, viwanja 

WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema kati ya Januari hadi Desemba mwaka jana, Watanzania wanaoishi nje ya nchi (diaspora) waliwekeza takribani Sh bilioni 4.4 katika ununuzi wa nyumba na viwanja.

Waziri wa wizara hiyo, Dk Stergomena Tax amesema hayo bungeni Dodoma jana wakati anawasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Dk Tax alisema diaspora walifanya uwekezaji huo kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kampuni ya Orange Tanzania Ltd (Hamidu City Park) na kampuni ya KC Land Development Plan Consultant Ltd.

Advertisement

Aliwaeleza wabunge kuwa uwekezaji huo ni sawa na ongezeko la Sh bilioni 2.2 zilizowekezwa katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2021.

“Vilevile, katika kipindi cha mwezi Januari hadi Desemba 2022, diaspora waliwekeza katika hisa za Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja (UTT – AMIS) zenye thamani ya takribani shilingi bilioni 2.5,” alisema Dk Tax.

Alisema kuanzia Januari hadi Desemba mwaka jana, diaspora walituma nyumbani takribani Dola za Marekani bilioni 1.1 kupitia vyanzo rasmi ikiwamo miamala ya kampuni za simu, benki na taasisi nyingine za fedha.

Dk Tax alisema fedha hizo ni takribani mara mbili ya dola za Marekani milioni 569.3 walizotuma kuanzia Januari hadi Desemba 2021.

Alisema wizara hiyo ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuwapatia hadhi maalumu diaspora wenye asili ya Tanzania na uraia wa nchi nyingine.

Dk Tax alisema wizara hiyo imekamilisha maandalizi ya mfumo wa kidijitali wa kukusanya na kutunza taarifa za diaspora na akasema utaiwezesha serikali kupata takwimu za idadi ya diaspora, mahali walipo, ujuzi na uzoefu wao.

Alisema pia mfumo huo utawawezesha diaspora kupata taarifa kuhusu fursa na huduma zinazotolewa na sekta za umma na binafsi nchini.

Dk Tax alisema wizara imeendelea kuhamasisha taasisi za umma na binafsi kuanzisha madawati ya diaspora ili kuongeza wigo wa huduma kwa Watanzania hao.

Alisema hadi sasa taasisi za serikali zilizoanzisha madawati ya huduma kwa diaspora ni Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Idara ya Uhamiaji Tanzania, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na NHC.