MWANAMUZIKI Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ amefunguka mengi kuhusu baba yake mzazi anayefahamika kwa jina la Mzee Omary Nyembo baada ya baadhi ya mashabiki zake kumbebesha lawama kuwa hamjali mzee wake huyo.
Hayo yaliibuka juzi baada ya mzee huyo kuhojiwa na Kituo cha Clouds akiwa Sumbawanga akieleza maisha anayoishi akitegemea biashara yake ya kuendesha bajaji mbili alizonunua baada ya kuacha kazi ya udereva wa magari makubwa.
Hata hivyo, wengi walionesha kutofurahishwa na biashara anayofanya mzee huyo ikilinganishwa na umaarufu wa Ommy na mazingira anayoishi yeye lakini jana msanii huyo ikiwa ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwake alieleza kilichojiri mpaka yeye na baba yake kuwa mbalimbali.
“Nilichokiona mimi wengi wanatakiwa kujifunza kwa wale ambao ni wazazi na wanaotarajiwa kuwa wazazi kwamba hakuna kitu bora utamtendea mtoto kama utamwonesha upendo, unamjali hata kama huna kitu, hicho ndiyo kitu pekee katika maisha yangu mimi nilikikosa.
“Nimelelewa kwenye maisha ambayo namwona mama tu mpaka nakua na bahati mbaya mama yangu alifariki wakati niko ‘primary’ lakini kwenye msiba baba sikumwona, hakunitafuta hata kunipa pole yaani alikimbia majukumu moja kwa moja, lakini leo mtoto ambaye sithaminiwi akaja kuwa mtu fulani na ndiyo sasa hivi kinachoendelea,” alisema Ommy.
Ommy anafafanua zaidi kuwa hayo yalimkuta kwa kuwa alikuwa ni mtoto wa nje ya ndoa, tofauti na watoto wengine 15 alionao na zaidi kwa sasa anataka atambulike zaidi kama Baba Ommy Dimpoz.
Msanii huyo anaeleza kuwa hajawahi kuwa na ukaribu na mzazi wake huyo wa aina yoyote na mara ya mwisho alionana naye takribani miaka 20 iliyopita na alimvunja moyo alipomwambia kuwa yupo mtoto mwingine mmoja kati ya hao 15, lakini kwa sasa hajui alipo ila akikua atamtafuta.