Dira ya Maendeleo 2050 kuwekeza rasilimaliwatu

WIZARA ya Fedha na Mipango imesema katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, taifa litawekeza nguvu kujenga na kuendeleza rasilimaliwatu.

Kamishina wa Mipango ya kitaifa katika Wizara ya Fedha na Mipango ambaye ni Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Maandalizi ya Dira hiyo, Dk Mursali Milanzi alisema hayo Dar es Salaam jana katika kikao cha kujadili maandalizi ya dira hiyo.

Alisema msukumo katika kilimo cha kisasa utawekwa katika matumizi ya mbegu bora za kisasa, umwagiliaji na kuzingatia mnyororo wa thamani pamoja na kufungamanisha kilimo na viwanda.

“Viwanda vikiimarika, wakulima watapata soko na viwanda hivyo nchini pia vitapata malighafi za kutosha na kirahisi na hiyo italeta tija kwa uchumi na maendeleo ya taifa na watu wake,” alisema na kuongeza:

“Hata sekta ya elimu tunataka iwe ya kisasa, vipaumbele ni kuzifanya sekta zote zikiwamo za kiuchumi na kijamii kuwa za kisasa,” alisema Milanzi.

Alisema katika mchakato wa maandalizi ya Dira ya 2050, sekretarieti na wadau wengine watatumia vyombo vya habari ikiwamo mitandao ya kijamii kupata maoni kuhusu dira mpya.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Natu El-Maamry Mwamba alisema katika mchakato huo wananchi watatoa maoni ili kupata dira itakayoleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii.

Aprili mwaka huu Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alizindua mchakato wa maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na akaagiza maandalizi yazingatie uimarishaji uwezo wa uchumi uliopo na kulinda mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.

Dk Mpango aliagiza maandalizi pia yazingatie suala la elimu hasa ya sayansi, ufundi na ufundi stadi, utafiti na maendeleo na ubunifu ili kukuza ujuzi na uwezo wa nguvu kazi ya taifa.

Aliagiza pia kuvutia na kuasili teknolojia ili kukuza tija katika sekta zote za uzalishaji na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Habari Zifananazo

Back to top button