DIT yaanza kutoa mafunzo ya matumizi ya vishikwambi kwa walimu

TAASISI ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imeanza kutoa mafunzo kwa walimu waliopatiwa vishikwambi. Aidha, imesema walimu hao pia wanapaswa kufundishwa namna ya kutengeneza vishikwambi hivyo pindi vitakapoharibika ili kuwe na matumizi endelevu badala ya kuvitelekeza.

Akizungumza Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Kituo cha Umahiri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa DIT, Dk Petro Pesha alisema lengo la serikali kugawa vishikwambi hivyo ni kuboresha mazingira ya ufundishaji na kuhamasisha matumizi ya teknolojia.

Alisema kuwa ili kuwe na matumizi endelevu ya vishikwambi hivyo, walimu wanapaswa kuvilinda na kuvitunza ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa.

“Tuliona mahitaji makubwa kwa walimu waliopewa vishikwambi, wako ambao hawajui jinsi ya kuvitumia wala kuvitengeneza pale vinapoharibika na badala yake huwaachia watoto wao wachezee,” alisema Dk Pesha.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe alisema lengo la kutolewa kwa vishikwambi hivyo ni kuboresha utoaji wa elimu nchini na kuwarahisishia kazi walimu. Alisema katika mapinduzi ya nne ya viwanda, ni lazima walimu waendelee kujifunza masuala mbalimbali ya Tehama ili kupata maarifa yatakayowasaidia katika kazi zao.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button