WIZARA ya Elimu Sayansi na Teknolojia imesema licha ya kuwepo kwa wanawake kujikita kwenye eneo la sayansi na teknolojia bado idadi haitoshi na kuiitaka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kuongeza udahili hususani kwenye eneo la uhandisi na teknolojia.
Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Profesa Peter Msofe amesema hayo leo Dar es Salaam wakati akisoma hotuba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Carolyne Nombo katika utoaji wa tuzo kwa wanafunzi waliofanya vyema katika masomo yao kwa mwaka 2022/23 chuoni hapo.
Amesema idadi ya wanawake wanaosomea masuala ya teknolojia ya sayansi wamekuwa wakiongezeka lakini sio kwa kiwango kikubwa hivyo ni vyema kushirikina katika nyanja mbalimbali ili kuongeza wigo katika eneo hilo.
Kuhusu tuzo amesema hutolewa kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao kuanzia ngazi ya cheti hadi uzamili lengo likiwa ni kuhamasisha na wanafunzi kuongeza juhudi katika masomo yao.
Amesema ni muhimu kwa DIT kuendelea kutoa tuzo hizo na kila mara waone namna ya kuziboresha ili wale wanaofanya vizuri katika masomo yao wapewe. Tuzo zinazotolewa ni pamoja na cheti, fedha hata nafasi za kufanya kazi kwa vitendo.
Amesema tuzo hizo zinahamasisha na kuwatambua wale wanaofanya vizuri jambo linalojenga ushindani, bidii na kujiamini huku akiwataka wanafunzi kuwajibika kusoma kwa bidii kwa kuwa ushindi humfikia anayejituma na mwenye nidhamu.
Msofe amesema alisisitiza wanafunzi kuruhusu fikra zao kufika mbali nje y akile wakionacho mara kwa mara wakihitaji mabadiliko chanya ili kuweza kufikia ndoto zao.
“Msiogope kutumia vipawa vyenu, kuweni wabunifu katika maeneo mbalimbali ambazo yanawezakubadilisha maisha na kuleta maendeleo kwenu na kwa taifa kwa ujumla,” amesema Profesa Msofe.
Awali akizungumza, Mkuu wa Taasisi ya DIT, Profesa . Preksedis Ndomba. amesema utaratibu wa kuwatuza wanafunzi chuoni hapo umekuwa ukiongeza ufaulu na ushindani miongoni mwa wanafunzi jambo ambalo limeibua hamasa kwa wanafunzi walio wengi.
Amesema awali chuo kilikuwa kikiwashindanisha wanafunzi kwa mfumo wa kuangalia ubora wa ufaulu (GPA) lakini ikaamua kuubadili na kuwatuza wale wanaofanya vizuri jambo lililosaidia kuleta hamasa ya kusoma.