DIT yatoa mafunzo ya Tehama bure kwa walimu    

TAKRIBANI walimu 100 wa shule za msingi wilayani Ilemela, mkoani hapa, wananufaika na mafunzo ya Tehama bila malipo katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Kampasi ya Mwanza, ili kuwawezesha kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Mafunzo hayo ni sehemu ya utaratibu wa Kampasi kurudisha kwa jamii kile inachovuna (CSR), wazo lililojitokeza baada ya walimu nchini kupewa vishikwambi na serikali, vilivyokua vikitumika wakati wa sensa ya watu na makazi mwaka jana.

Mhadiri wa Kampasi, Shija Mbitila, amesema mafunzo hayo ya wiki nne kuanzia Machi 22, yatawawezesha walimu kumudu ipasavyo matumizi ya vishikwambi hivyo, ili kurahisisha kazi zao, ikiwemo kufanya maandalio ya masomo, pamoja na kuandaa mitihani na matokeo.

“Walimu ni moja ya makundi muhimu katika jamii yanayopaswa  kumudu kasi ya mabadiliko ya teknolojia, tukaamua kutoa masomo haya bure, ambayo kimsingi kila mwanafunzi hulipia Shilingi 120, 000,” amesema.

Mshiriki wa mafunzo, Mwalimu Neuster Kamugisha wa shule ya Msingi Mwambani, amepongeza jitihada za taasisi, akasema binafsi hajawahi kutumia kompyuta toka kuzaliwa kwake.

Amesema yeye na wenzake mara nyingi wamekua wakitumia vishikwambi hivyo kama simu tu, kupiga, kupokea na kutuma ujumbe mfupi, lakini hawana ujuzi wa kutumia progamu zingine zilizomo.

“Kupitia mafunzo haya, sasa tunaweza kuchapa na kuhifadhi nyaraka kwenye vishikwambi, pamoja na kutumia programu ya ‘Excel’ ambayo itatusaidia hasa kupanga matokeo ya mitihani ya wanafunzi,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button