Diwani matatani kukodisha, kuuza mashamba ya kijiji

TABORA: WANANCHI wa Kijiji cha Iborogero na Kata ya Iborogero Wilaya ya Igunga mkoani Tabora wamemtuhumu Diwani wa kata hiyo, Emmanuel Bundara kwa kukodisha na kuuza mashamba ya serikali ya kijiji hicho.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye maeneo ya mashamba hayo yaliyopo jirani na Shule ya Sekondari Iborogero, baadhi ya wananchi hao; Philipo Matoke, Mwita Wambura na Milembe Shija wamesema tangu diwani huyo wamchague amekuwa kikwazo cha kutothamini mali za serikali ikiwemo mashamba.

Wamesema serikali ya kijiji hicho ina eneo la mashamba lenye ekari zaidi ya 200 ambapo diwani huyo amekuwa akikodisha maeneo hayo kwa baadhi ya wananchi kuanzia Sh 40,000 hadi Sh 100,000 kwa kukata vipande vidogo vidogo.

Wambura amesema wakati akikodisha mashamba hayo pia mengine amekuwa akiuza kwa wananchi wa Kata ya Ziba kwa bei ya Sh 500,000 kwa ekari moja ambapo tayari Peter Kulaba na Maganga Sululi amewauzia ekari moja moja kwa thamani ya Sh milioni moja.

Kutokana na hali hiyo, wamemwomba Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Sauda Mtondoo na Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Igunga kuchukua hatua za haraka dhidi ya diwani huyo kwani bila hivyo mashamba ya kijiji yataendelea kuuzwa.

Naye Mtendaji wa kijiji hicho, Juma Mayunga alipoulizwa alisema diwani huyo amekuwa hashauriki na kuingilia masuala ya serikali ya kijiji.

Kwa upande wake, diwani huyo Bundara alipoulizwa juu ya tuhuma hizo alisema yeye hajawahi kuuza au kukodisha mashamba ya serikali ya kijiji wala kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Sauda Mtondoo alithibitisha kupokea malalamiko toka kwa wananchi dhidi ya diwani huyo na kusema kuwa alishamuita ofisini kwake pamoja na viongozi wa serikali ya kijiji akawakanya tabia ya kuuza maeneo hayo.

Alisema kwa kuwa suala hili limejirudia tena atachukua hatua kali za kisheria.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button