KATIBU Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbasi amesema anatamani kuona Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), inakuwa taasisi ya mfano kwa kuwa na mafanikio makubwa katika utendaji na utekelezaji wa majukumu yake.
Dk Abbasi amesema hayo Aprili 06, 2023 akizungumza na Menejimenti ya TAWA wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya kwenye Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka hiyo mkoani Morogoro.
Amesema ili kufikia mafanikio makubwa katika Mamlaka hiyo, mambo manane yanapaswa kuzingatiwa na Mamlaka katika kusaidia kufikia malengo hayo.
Ameongeza kuwa mamlaka hiyo inapaswa na malengo makubwa “Olympic Targets” tofauti na malengo ya kawaida na kuyatekeleza kwa ufanisi.
Dk Abbasi ametaja jambo lingine ni pamoja na kufanya kazi kama timu na kufuata maadili ya utumishi wa Umma katika kuhakikisha Mamlaka inakuwa na mafanikio makubwa katika kila nyanja.
Pamoja na hayo ameitaka Menejimenti ya Mamlaka hiyo kuwekeza vya kutosha katika kitengo cha Mawasiliano kwa kuhakikisha kinapata mahitaji ya msingi kama vile vitendea kazi vya kutosha ili kupata matokeo yanayotarajiwa.
Katibu mkuu pia amewataka watumishi wa Mamlaka hiyo kumtanguliza Mungu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili kuongeza ufanisi wao katika maeneo yao ya kazi .
Dk Abbasi amesema falsafa ya Wizara ya Maliasili na Utalii imejikita katika kuhifadhi rasilimali zilizopo Nchini na kutangaza vivutio vyote vya Utalii vilivyopo nchini.
“Ninaagiza watumishi wote wa Wizara hii kuongeza kasi ya utekelezaji wa falsafa hii”amesisitiza Dk Abbasi