Dk Bashiru: Njaa inatweza utu

Ataka ubunifu kukabili mfumuko wa bei 

MBUNGE wa kuteuliwa Balozi Dk  Bashiru Ally Kakurwa amesema mfumuko wa bei ya vyakula unasababisha wananchi kupiga pasi ndefu na kwamba njaa inatweza utu wa mtu
Dk Bashiru ameyasema hayo  akichangia katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo mifugo na maji, bungeni mjini Dodoma leo  Januari 31,2023
Amesema  njaa inadhalilisha heshima na uhuru wa nchi, njaa inatweza utu wa mtu hivyo tatizo la mfumuko wa bei za vyakula ni tatizo ambalo lazima kuongeza kiwango cha ubunifu
“Kutokana na mfumuko wa bei wananchi inabidi wapige pasi ndefu yaani chai ya asubuhi inanyweka kati ya saa  tano na saa sita, na cha mchana kinaliwa kati ya saa 11 na saa 12, hii inafanyika ili kukabiliana na mfumuko wa bei.
Amesema, kama wananchi wanakua wabunifu katika kupambana na maisha , serikali haina budi kuongeza wigo wa ubunifu ili kukabiliana na mfumuko wa bei za vyakula
 Aidha, Dk Bashiru akihitimisha maoni yake aliacha  maswali kama ifuatavyo je ruzuku ya mbolea, mafuta, mbegu imepunguza makali kiasi gani ya mfumuko wa bei ya vyakula?
Je kutokuwa na ‘Lockdown’ kumepunguza kiasi gani makali ya mfumuko wa bei ya vyakula?
Je udhibiti wa kuuza vyakula nje ukiwepo unamnufaisha nani na vyakula vikiuzwa nje hiyo ruhusa inamnufaisha nani?
Kauli ya Dk Bashiru imekuja kukiwa na mfumuko mkubwa wa bei kilo ya Maharage ikiuzwa sh 4000 kutoka Shilingi 2000 hadi 2500 huku kilo la mchele ikiuzwa kati ya 3800 na 4,500
Kwa mujibu wa NBS, mfumuko wa bei wa jumla ulikua asilimia 4.3 mwaka 2022 ukilinganisha na asilimia 3.7 mwaka 2021 na asilimia 3.3 mwaka 2020.
Kuna ongezeko la bei za vyakula,mathalan, gunia la kilo 100   mchele linauzwa kwa wastani wa Sh312,921 ukilinganisha na Sh202,353 mwaka jana.
Gunia la maharage limefikia Sh318,947, ongezeko la asilimia 55 ya ile ya mwaka jana iliyokuwa Sh203,118 kwa mujibu wa ripoti ya bei za vyakula ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Habari Zifananazo

Back to top button