Dk Biteko ahimiza usimamizi bora wa Ilani

NAIBU Waziri Mkuu, Waziri wa Nishati na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dk Dotto Biteko amewataka viongozi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujikita zaidi katika kusimamia Ilani ya chama na kuachana na siasa za chuki.

Dk Biteko amesema hayo katika mkutano wa hadhara kwenye kata ya Namonge wilayani Bukombe na kueleza viongozi wanapaswa kutambua CCM ndio imepewa dhamana ya kuongoza nchi.

“Shughulikeni na tupambane na shida za watu, watani zetu watafika watatukana tusirudishe, watafika watasema hatujafanya kitu, tusihangaike kuwaonyesha tumefanya nini, wananchi wanaona.

Advertisement

“Tukiamuka asubuhi tuwaze shida za watu, tutatue shida za watu, mahali ambapo kuna malalamiko ya shida za watu, tusisubiri mkuu wa wilaya aje, viongozi wa eneo hilo tumalize shida hizo.” Amesema na kuongeza;

“Tusisubiri mkuu wa mkoa aje, tumalize hizo shida kabla mkuu wa mkoa hajaja, wala mkoa msisubiri Rais aje, sisi tuzimalize shida za watu, watanzania wanachohitaji ni maendeleo.”

Amesema usimamizi thabiti wa ilani ya CCM utawezesha maboresho ya miundombinu ya barabara na huduma ya maji, elimu na afya ambazo ndio mihimili ya maendeleo kwenye jamii ya wananchi wa kawaida.

“Niwaombe watu wa CCM, nendeni hata kwa mtu wa Chadema kama ana shida wala msiwachukie, wakati mkiwaonyesha wema, mtawageuza mioyo yao, watu wa Bukombe ushindeni ubaya kwa wema.

“Msilipe ubaya kwa ubaya mkitendewa ubaya msamehe mkitendewa jema mshukuru, na yoyote atakayewapuuza msameheni lakini tushughulike na shida za watu, hatutapimwa kwa kusema tutapimwa kwa matokeo.”

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *