Dk Biteko aipongeza REA umeme vijiji vya Iringa

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko amewasha umeme katika kijiji cha Mkangwe wilayani Mufindi kama pongezi ya mabadiliko chanya yaliyofanywa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika kuhitimisha shughuli ya kuviunganisha vijiji vyote 360 vya mkoa wa Iringa na nishati hiyo.

Kwa mujibu wa Dk Biteko, mtandao wa umeme katika vijiji vyote vya mkoa huo unatarajiwa kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii katika jamii hizo ambazo huduma ya nishati hiyo kwao ilikuwa historia.

Dk Biteko alisema umeme unaweza kuwezesha shughuli za kiuchumi vijijini kama vile kilimo, biashara ndogo ndogo, na viwanda vidogo, hivyo kusaidia kuinua hali ya maisha na kukuza uchumi wa maeneo hayo.

Advertisement

Lakini pia alisema umeme unaweza kuboresha upatikanaji wa elimu kwa kutoa nishati ya kutosha kwa shule, kuwezesha matumizi ya kompyuta, na kusaidia upatikanaji wa habari kupitia vyanzo vya umeme.

Mengine ni pamoja na kuboresha huduma za afya kwa kuwezesha matumizi ya vifaa vya matibabu na kuimarisha mfumo wa kuhifadhi dawa na chanjo, kuimarisha mawasiliano, kupunguza utegemezi wa nishati nyingine kama mkaa na kuni, kukuza ujasiriamali na kuboresha usalama.

“Hii ni habari nzuri. Kusambaza umeme vijijini ni hatua muhimu kwa maendeleo na ustawi wa jamii. Tunamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake njema kwa wananchi wa vijijini na tunaipongeza REA kwa kusimamia miradi hii kama inavyokusudiwa,” alisema.

Alisema mafanikio hayo ni matokeo ya kazi kubwa inayofanywa na serikali ya awamu ya sita inayolenga kuhakikisha huduma zote muhimu zinafika kwa wananchi katika maeneo yote nchini.

“Nataka niwaambie wana Iringa mambo haya hayaji kwa bahati mbaya, ni sehemu ya mafanikio ya kuwa na serikali na chama kinachosikiliza na kutatua matatizo ya wananchi; dhamira ya Rais wetu ni kuhakikisha kila kitongoji kinapata umeme”, amesema.

Dk Biteko ameiagiza REA kuwachukulia hatua ikiwemo kuwanyang’anya miradi wakandarasi wanaosuasua katika utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme.

“Ni muhimu kuhakikisha kuwa miradi ya umeme inatekelezwa kwa uwazi na kwa ubora unaozingatia thamani ya fedha inayotolewa na serikali ili ilete athari chanya kwa jamii,” alisema.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango wa kusambaza umeme mkoani humo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dendego alisema hadi kufikia Disemba, 2023 vijiji vyote vya mkoa huo vilikuwa tayari vimefikiwa na huduma hiyo kwa asilimia 100.

Akizungumzia usambazaji wa umeme katika vitongoji vya vijiji, Dendego alisema shughuli hiyo imefanyika kwa asilimia 64. 11 ambayo ni sawa na vitongoji 1,188 kati ya vitongoji vyote 1,853.

Sambamba na kuzindua umeme katika kijiji cha Mkangwe, Dk Biteko amezindua pia zahanati ya kijiji hicho huku akiuagiza uongozi wa halmashauri ya wilayani Mufindi kuhakikisha inaanza kuhudumia wananchi kuanzia Februari 26, mwaka huu.