Dk Biteko: Rais Samia ni kiigizo cha maridhiano

KAGERA: NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko Biteko amewataka viongozi wa nafasi mbalimbali nchini kufanya kazi  na watu wanaowaunga mkono na wasiowaunga mkono kwani wajibu wao ni kuwahudumia wananchi wote.

Katika hotuba yake, Dk Biteko amemtolea mfano Rais Samia Suluhu Hassan kuwa ni Muumini namba Moja wa maridhiano nchini na haishii katika kusema tu bali anatekeleza kwa vitendo huku nia ikiwa ni kuhakikisha kunakuwa na umoja na amani nchini.

 

Dk Biteko amesema hayo leo wakati wa Misa Maalum ya Kutabaruku Kanisa Kuu la Kiinjili la Kilutheri Tanzania ( KKKT) Lukajange, Dayosisi ya Karagwe iliyofanyika wilayani Karagwe, Mkoa wa Kagera. Misa hiyo maalum imehudhuriwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi ( CCM), Bara, Komredi Abdulrahman Kinana , Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa.

“Rais, Dk Samia anasema kila mara kuwa hii nchi ni yetu sote, anatuasa mara nyingi kuwa wewe kama ni CCM mpende Mpinzani, na Mpinzani mpende CCM, tuungane pamoja tusukume nchi yetu mbele, na hakuishia hapo tu, akaunda Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano ambayo  imejumuisha makundi mbalimbali wakiwemo wanasiasa kutoka Vyama mbalimbali na viongozi wa dini ili kuwe na muafaka nchini, tujenge Tanzania bora kwa ajili yetu na vizazi vijavyo,” amesisitiza Dk Biteko

 

Kwa upande wake,Komredi Kinana amempongeza Askofu Benson Bagonza kwa uongozi mzuri katika Dayosisi ya Karagwe na ujenzi wa Kanisa Kuu jipya katika Dayosisi hiyo. Pia amewapongeza Mashemasi Watano katika Dayosisi hiyo ambao wamepata Uchungaji.

Waziri wa Ujenzi, ambaye pia ni Mbunge wa Karagwe, Innocent Bashungwa  amepongeza pia kwa ujenzi wa Kanisa hilo Kuu na pia amempongeza Askofu Benson  Bagonza kwa kufanya kanisa katika Dayosisi hiyo kuzidi kusonga mbele.  Pia ameahidi kushirikiana nao katika kujenga Dayosisi hiyo.

Kwa upande wake, Askofu wa Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia  suala la maridhiano kwa makundi yanayoonesha kukinzana huku akisema kuwa upatanisho huo anaousimamia una baraka za Mungu na amemtia moyo wa kuendelea kusimamia maridhiano kwani ni Afya ya Taifa.

Aidha, amemshukuru Rais Samia, pamoja na  viongozi mbalimbali wa Serikali waliochangia ujenzi wa Kanisa Kuu la KKKT, Dayosisi ya Karagwe pamoja na waumini na wadau mbalimbali.

 

Pia, Askofu Bagonza ametoa pole kwa Serikali na Wananchi kufuatia vifo na majeruhi vilivyotokana na janga la kiasili wilayani Hanang, mkoani Manyara.

 

Dayosisi ya Karagwe ilizinduliwa mwaka 1979 ambapo ujenzi wa Kanisa hilo kuu ulianza mwezi Februari 24, 2023 na kukamilika mwezi Novemba 2023. Ujenzi wa Kanisa hilo umegharimu  Shilingi milioni 400.

Habari Zifananazo

2 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button