DAR ES SALAM: NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amewataka watendaji wakuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) kuacha alama katika utendaji wao kwa kuwashika mkono na kuwapandisha wale waliopo chini yao.
Dk Biteko ameyasema hayo Oktoba 26,2023 katika Maadhimisho ya Miaka 40 ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) yaliyofanyika katika ukumbi wa APC Bunju jijini Dar es Salaam.
Amesema, kuadhimisha miaka 40 ni miaka mingi sio tu kufurahi kwa sababu ya kupata mafanikio makubwa wanatakiwa kigeuka nyuma na kuangalia walipotoka na kujifuza kwa viongozi waliokuwepo katika taasisi hiyo.
“Wametuonyesha ugumu waliopitia na mambonde waliyoyapitia, milima waliyoipitia na mafanikio waliyoyapata nimepata uzoefu mkubwa kutoka kwa Profesa Bwathon Philip ambaye ni mwanzilishi wa kwanza wa taasisi hii ametufundisha mambo mengi ya uongozi na usimamizi wa taasisi,”amesema Biteko.
“Nataka kuwambia madarakani mliyopewa, hakikisheni mnawashika mikono waliopo chini yenu, mnawajenga wakue kama mlivyojengwa nyinyi, hata mkiondoka mfurahie matunda ya wale mliowashika mkono, jitahidini kuacha vitu vilivyo hai na sio makaburi.”Amesema Biteko
Kauli ya Biteko imekuja kufuatia historia iliyotolewa na Mkurugenzi wa kwanza wa TAFIRI Profesa Bwathon Philip akielezea changamoto walizokumbana nazo hadi kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 1980 baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mwaka 1977.
Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema kuwa, wizara imehakikisha Sekta ya Uvuvi inakuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa na amesisitiza kuwa Sekta hiyo inaweka mazingira mazuri ili kuvutia uwekezaji na wavuvi wanufaike na rasilimali hiyo.
Katika hatua nyingine, Ulega amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha takriban Sh bilioni 25 kwa ajili ya kusaidia Sekta ya Uvuvi nchini.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TAFIRI, Dk Ismael Kimirei alisema kuwa taasisi yake kupitia mfumo huo mpya wa upatikanaji wa taarifa kwa wavuvi utawasaidia wavuvi kujua makundi ya samaki yaliyopo kupitia simu zao na kuachana na uvuvi wa kubahatisha. Ameongeza kuwa, taasisi hiyo ni muhimili muhimu katika Sekta ya Uvuvi.
Comments are closed.