DK Biteko: Watanzania wanahitaji mafuta kwa urahisi
DAR ES SALAAM: Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema Watanzania wanahitaji wapate mafuta kwa urahisi ili shughuli za kiuchumi na kijamii zifanyike kujenga uchumi wa nchi.
Hayo yameelezwa leo Oktoba 27, 2023 na Dk. Biteko alipotembelea gati la kupokelea mafuta (KOJ), eneo la Kigamboni zinapojengwa mita mpya za kupimia uingiaji wa mafuta (Flow meter) za Serikali zinazosimamiwa na TPA na matenki ya kuhifadhia mafuta yanayomilikiwa na kampuni ya TIPER jijini Dar es Salaam.
” Wananchi wapate mafuta kwa urahisi lakini pia kwa bei rafiki sio kunakuwa na ucheleweshwaji wa kupata mafuta kwa sababu zilizo ndani ya uwezo wetu,” amesema Dk. Biteko.
Aidha, Dk. Biteko ameridhishwa na utaratibu wa upokeaji na upakiaji mafuta kuwa unaendelea vizuri na kusisitiza changamoto chache zilizopo zinaendelea kushugulikiwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).
Akizungumza upande wa TIPER amesema kuwa, ameanza kupokea mafuta na ameonyesha uwezo mkubwa wa kupokea na kusambaza mafuta kupeleka kwa wateja. Pia, amesema ujenzi wa matenki mapya ya kuhifadhia mafuta eneo la TIPER utaongeza ufanisi na kupunguza gharama za kusubiri ambazo zinachangia gharama ya mafuta kwa mwananchi.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya TIPER, Mohamed Mohamed ameahidi kuwa, kampuni hiyo itaendelea kuboresha miundombinu ya kupokea na kusambaza mafuta ili kuongeza ufanisi zaidi.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, aliambatana na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi. Felchesmi Mramba, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo, Meneja wa Bandari ya TPA Dar es Salaam, Mrisho Mrisho, wawakilishi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), TRA na Wataalam kutoka Wizara ya Nishati.