Dk Chana aifariji familia askari aliyeuawa Serengeti

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk Pindi Chana, ametoa salamu za pole kwa familia ya marehemu Deus Mwakajegele, askari wa uhifadhi aliyekuwa akifanya kazi Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ambaye alichomwa mshale wenye sumu wakati akitekeleza majukumu yake eneo la Nyanungu, Wilaya Tarime mkoani Mara.

Waziri Chana ametoa salamu hizo leo Alhamisi Januari 26, 2023, alipofika nyumbani kwa marehemu eneo la Ngongongale wilayani Arumeru mkoani Arusha, kufuatia kuguswa na kifo cha askari huyo, ambaye enzi za uhai wake alijitoa kulinda wanyamapori kwa niaba ya Watanzania.

”Mimi kama Waziri mwenye dhamana ya maliasili na utalii, nimekuja hapa kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na jumuiya yote ya wahifadhi.

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha kijana wetu aliyeshambuliwa kwa kupigwa mshale wenye sumu na watu wasiojulikana Januari 21, 2023 wakati akitekeleza majukumu yake,” ameeleza Dk  Chana.

Kufuatia hali hiyo, Waziri Chana amekemea vikali vitendo  vya baadhi ya wananchi wanaojichukulia sheria mkononi, huku akisisitiza kuwa Jeshi la Uhifadhi liko imara na litaendelea kulinda maeneo yote ya hifadhi kwa faida na manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

Katika hatua nyingine Waziri Chana amebainisha kuwa mtu aliyedaiwa kuhusika na tukio lililosababisha kifo cha askari huyo tayari ameshamakatwa, huku watuhumiwa wengine waliohusika na tukio hilo wakiendelea kusakwa ili sheria ichukue mkondo wake.

Kwa upande wake mjomba wa marehemu, Sisito Kigongo ameeleza kuwa askari huyo alikuwa ni mhimili kwa familia, hivyo kifo chake kimekuwa pigo kubwa kwa  familia, huku akibainisha kuwa marehemu ameacha watoto watatu.

Habari Zifananazo

Back to top button