Dk Chana ataka ubunifu TFS

Dk Chana ataka ubunifu TFS

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk Pindi Chana amewaasa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuongeza ubunifu na kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazojitokeza wakati huu ikiwemo ya kuwekeza katika biashara ya kuvuna hewa ukaa.

Balozi Dk Chana alitoa agizo hilo Jumatatu Dodoma wakati akifungua mkutano wa kwanza wa makamanda wa vituo vya TFS.

Balozi Chana aliwaasa pia wachangamkie fursa za miradi ya kimataifa itakayosaidia kuongezea rasilimali fedha zitakazosaidia katika kuleta ufanisi na kuendeleza sekta hiyo ya misitu nchini.

Advertisement

Aliwapongeza TFS kwa kuongeza makusanyo ya maduhuli mwaka jana 2021/22 walikusanya bilioni 157.

8 sawa na asilimia 102.04, akawataka waendelee kuweka mikakati ya kukusanya zaidi.

Dk Chana aliwapongeza TFS kwa kununua vifaa vya kuboresha utendaji kazi kila mwaka, katika kipindi cha miaka miwili wamejenga nyumba mpya 62 na kununua vifaa vya ulinzi na mitambo 78, pikipiki 100 za doria, kwa kufanya hivyo kunawatia moyo makamanda na kuleta motisha katika kufanya kazi kwa ufanisi.

Aliwaagiza wazuie migogoro mipya isitokee katika maeneo yakiwemo ambayo Kamati Maalumu ya Mawaziri wanane ilipita na kuona migogoro.

Aliwataka makamanda hao kusimamia kikamilifu na kuhakikisha changamoto za uvamizi misitu kwa kuingiza mifugo au kulima mashamba, haitokei tena.

Kamishna wa Uhifadhi TFS, Profesa Dosantos Silayo alimwomba waziri kukamilisha na kupata mrejesho wa ripoti ya Kamati ya Mawaziri Wanane iliyopita katika maeneo ili kumaliza changamoto ya migogoro mipaka baina ya wakala na wananchi.