Dk Kapologwe ataka uwazi, uwajibikaji
MKURUGENZI wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Dkt. Ntuli Kapologwe amesisitiza kuwepo kwa uwazi na uwajibikaji katika ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya unaoendelea kwa kasi nchi nzima.
Ametoa msisitizo huo leo wakati akikagua ujenzi wa miundombinu katika kituo cha afya cha Sima wilayani Sengerema,mkoani Mwanza.
Amesema, serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imetoa zaidi ya sh bilioni 900 ili kujenga na kuboresha Hospitali,zahanati na vituo vya afya nchi nzima , kikiwemo kituo cha afya cha Sima.
“Tunataka kuona thamani ya fedha katika ujenzi huu kwani Serikali imeshaleta milioni 250, hivyo ujenzi ulipaswa kuwa umekamilika tangu mwezi disemba mwaka jana”, Dkt. Kapologwe amesisitiza.
Naye, mbunge wa jimbo la Sengerema Hamis Tabasamu ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa jitihada za kuboresha huduma za afya wilayani Sengerema na kuomba kuongezewa vifaa tiba ili kuendelea kuboresha zaidi utoaji wa huduma.