Dk Kiruswa atoa maelekezo 5 sekta ya madini

ARUSHA; NAIBU Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa, ametoa maelekezo matano kwa Tume na wadau wa sekta ya madini nchini.

Akifunga Jukwaa la Tatu la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini leo Mei 24, 2024 kwenye Ukumbi wa AICC jijini Arusha, Dk Kiruswa ameelekeza  Watanzania kujengewa uwezo, ili kuendana na soko la ajira katika sekta ya viwanda.

Amesema Tanzania imefungua milango ya uwekezaji katika sekta hiyo, ikiwemo kuendeleza ushirikiano na wadau wa madini, ili kufanikisha utekelezaji wa mikakati ya Vision 2030 ya madini ni maisha na utajiri, hivyo ni muhimu viwanda vinavyojengwa kwenye migodi viende sambamba na kuwapa ujuzi Watanzania.

“Ujenzi wa viwanda kwenye migodi, vinahitaji ujuzi sio kuanzisha tu, nitoe wito uanzishwaji wa viwanda uende sambamba na Watanzania kujengewa uwezo,”amesema Dk Kiruswa.

Agizo la pili amelitoa kwa wawekezaji wa migodi kutoa udhamini kwa mafunzo yanayofanyika nje ya nchi kwa watumishi wao ili kuwajengea uwezo.

Pia Dk Kiruswa ameagiza vyuo kufungamanishwa na wawekezaji wa viwanda ikiwemo kuandaa mitaala, ili kuendana na mahitaji ya soko husika.

Dk Kiruswa pia ameagiza kuanzishwa kwa programu maalum za kubadilishana uzoefu na mataifa mengine ‘Exchange Program’, ili kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani.

“Kuna umuhimu kwa wenye viwanda kutoa fursa kwa vijana wa vyuo kufanya mafunzo kwa vitendo kwenye viwanda vyao ili wapate ujuzi,”amesisitiza

Amesema kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, ili kuvutia uwekezaji zaidi hususan katika sekta ya viwanda vya bidhaa za migodini.

Amesema kuwa, Jukwaa hilo la Ushirikishwaji wa Watanzania lenye kauli mbiu ‘Uwekezaji wa Viwanda vya Uzalishaji wa Bidhaa za Migodini kwa Maendeleo Endelevu’ ni muhimu kwa wadau wa Sekta ya Madini kulitumia kama njia ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa miradi wanayoisimamia, ili kuchochea uwekezaji.

“Ni matumaini yangu kuwa kutakuwa na mabadiliko makubwa katika utekelezaji wa suala la ushirikishwaji wa Watanzania kwa wamiliki wa leseni na watoa huduma katika sekta ya madini nchini,”amesema Dk Kiruswa

Awali Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa jumla ya mada saba zimewasilishwa katika jukwaa hilo lililoanza rasmi Mei 22, 2024.

“Mada zote lengo ni uchechemuzi wa kuanzishwa viwanda hapa nchini na bidhaa zote zinazohitajika migodini zipatikane hapa hapa nchini, tunaposema kuna ongezeko la Watanzania kupata fursa katika sekta ya madini ambalo kwa sasa limefikia asilimia 84 na miaka michache ijayo tutafikia asilimia 100, lakini ni fursa zipi tunazozifikia?”Amehoji na kuongeza:

“Changamoto kubwa malighafi bado zinatoka nje ya nchi, fursa iliyopo sasa ni kujenga viwanda hapa hapa nchini, teknolojia za kisasa na bidhaa zinazotumika kwa wingi migodini zitoke hapa hapa nchini, serikali, watu binafsi tunawajibika kushirikiana ili kutimiza ajenda ya Vision 2030,”amesisitiza Mhandisi Samamba.

 

Habari Zifananazo

Back to top button