Dk Lwaitama azidi kufunguka kesi ya Mdee, wenzake

MJUMBE wa Bodi ya wadhamini ya Chadema, Profesa Azaveri Lwaitama amesema chama hiko hakikuwa na nafasi ya kuwapa muda zaidi mbunge, Halima Mdee na wenzake 18 kujieleza kwa kuwa kulikuwa na mvutano unaoendelea ndani ya chama hicho.

Alisema kuwa maamuzi yalikuwa lazima yafanyike haraka kwa ajili ya uhai wa chama kwa wakati huo.

Lwaitama alieleza hayo jana mbele ya Jaji, Cyprian Mkeha katika Mahakama kuu, Masjala kuu wakati wa kusikilizwa kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na wabunge wa viti Maalumu wa Chadema, Mdee na wenzake.

Advertisement

Akijibu kwa jazba swali la dodoso kutoka kwa mmoja wa Mawakili wa Mdee na mwenzake, Ipilinga Panya aliyeuliza ni kwa nini Halima na wenzake hawakupatiwa muda wa kujieleza kabla ya kufukuzwa uanachama, Lwaitama alisema kuwa walipewa nafasi ya kusikilizwa na kamati kuu lakini walidharau wito.

Aliieleza mahakama kuwa wabunge hao hawakufika mbele ya kamati na wala hawakutuma wawakilishi badala yake waliandika barua za kuomba kuongezewa siku saba mbele ili kusikilizwa na kamati hiyo huku wakitaja sababu ambazo hazikuwa na mashiko.

Alidai katika barua zao wote waliandika sababu ambazo zinazofanana wakiomba kuongezewa muda kutafakari tuhuma ambazo walikuwa wanakabiliwa nazo pamoja na kuhofia usalama wao.

Alidai moja ya barua hizo zilieleza kuwa anahofia kufika mbele ya kamati siku hiyo kufuatia ujumbe uliokuwa ukitumwa na mtu wa hamasa ukiwataka wanachama kufika kwa wingi makao makuu siku ambayo wabunge hao waliitwa mbele ya kamati.

Alisema kutokana na sababu hiyo chama kilibadili sehemu ya kukutana na wabunge hao lakini pia hawakufika kwa makusudi kwa kuwa walijua chama kitatoa maamuzi na baade ionekane kuwa hawakusikilizwa.

Alidai kuwa yeye alikuwa nje ya mkoa lakini alifanya jitihada zote kuhakikisha anafika makao makuu kuwasikiliza wabunge hao baada ya kupata wito wa chama.

“Mimi nimekaa uwanja wa ndege zaidi ya masaa (saa) sita kuhakikisha nawahi lakini cha kushangaza mimi nilifika katika muda uliopangwa lakini wao wahusika hawakufika na hata hawakutuma mwakilishi” alisema Lwaitama.

Alisema Mdee na wenzake walijua ni mwito wa dharura na hakuwa na sababu ya kuogopa kwenda kusikilizwa na labda kamati ingewaelewa na kubadili maamuzi yao ikiwemo kuwavua uwanachama.

Alisema sanjari na mwito huo Chadema ilijitahidi kuhakikisha Halima na wenzake wanarudi katika mstari ikiwemo mwenyekiti, Freeman Mbowe kuzungumza na Halima kama kiongozi na mtu mwenye ushawishi kwa wenzake lakini jitihada hazikuzaa matunda.

Alisema Chadema haipingi Halima na wenzake kuwa wabunge bali wanapinga utaratibu ambao umetumika wao kuingia bungeni na kusema kuwa yeye atakuwa mstari wa mbele kuwatetea warudishiwe uanachama iwapo watajitoa wenyewe bungeni.

Katika shauri hilo wabunge hao pamoja na mambo mengine waliiomba mahakama hiyo ipitie mchakato na uamuzi wa kuwafukuza uanachama kisha itoe amri zifuatazo.

Mosi itengue uamuzi wa kuwavua uanachama, pili iwalazimishe Chadema kuwapa haki ya kuwasikiliza pamoja na kutoa zuio dhidi ya Spika na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutochukua hatua yoyote mpaka malalamiko yao yatakapotolewa uamuzi.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *