Dk Mabula aonya watumishi wanaochomoa nyaraka za wateja

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angelina Mabula ametoa onyo kwa watumishi wa Jiji la Dodoma wanaochomoa nyaraka za wananchi.

Dk Mabula alitoa onyo hilo alipokutana na wananchi waliokumbana na changamoto katika mchakato wa kupata namba ya malipo ili kupata hati akitekeleza agizo la Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo aliyotoa wakati wa ziara yake mkoani Dodoma.

Hivi karibuni Chongolo alifanya ziara ya siku 10 katika wilaya za Mkoa wa Dodoma na kuagiza kushughulikiwa kwa changamoto ya migogoro ya ardhi ambayo imekithiri mkoani humo.

Advertisement

Alisema migogoro hiyo haitoki mbinguni na kuagiza kusakwa wanaosababisha migogoro hiyo ili wachukuliwe hatua. Mabula alitoa onyo baada ya kubainika mwananchi Shemaya Bihopho amecheleweshewa hati na kusababisha kiwanja chake kimoja kupewa mtu mwingine ambaye tayari ana hati.

“Sikutaka kuzungumza awali, lakini nina taarifa za kina za watumishi wa jiji ambao wanachomoa nyaraka za wananchi, wanaweka nyaraka zingine na wanarudisha tarehe nyuma na baadaye kuuza kiwanja kwa watu wengine. “Kesi hizo zipo nilikuwa nataka nipate ushahidi wa hata mtu mmoja tu, taarifa hizo ninazo. Niwahakikishie tutafuatilia mmoja baada ya mwingine ili wachukuliwe hatua,” alisema.

Pia Dk Mabula aliagiza Mkurugenzi wa jiji kufuatilia kwa kiwanja ambacho ofisa wa jiji aliagiza umiliki uende kwa mtu mwingine wakati mwingine anadai ni chake.

Akizungumza kabla ya kuanza kuwasikiliza wananchi, Dk Mabula alisema changamoto za ardhi katika Jiji la Dodoma ni mgogoro wa fidia za kiwanja, upimaji shirikishi ambao haukufanywa vizuri, kumilikishwa zaidi ya mara mbili, kutotekeleza ahadi ya kutatua migogoro, uelewa duni wa wananchi kuhusu wapi wafuate kutatua changamoto za ardhi.

Alisema serikali iliwaondoa vibarua zaidi ya 120 ambao walikuwa hawapokei mshahara, hawalipwi posho na hawana mikataba lakini ni mabosi kwenye Jiji la Dodoma katika ofisi ya halmashauri. Alimuagiza mkurugenzi wa jiji kuhakikisha ajira zote za mkataba zinafuata sheria na kuhakikisha wanawafanyia usahili huku akisisitiza wahakikishe wanachukua sura mpya.

Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo alisema mpaka sasa kuna viwanja 3,995 ambavyo wananchi wanapaswa kufidiwa na kuwa mkakati uliopo ni kuwa watatumia viwanja vilivyopimwa Nala viwanja 1,037.

“Kwa wale watakaokuwa bado hawajafidiwa, halmashauri ina mpango wa kupima viwanja 6,000 na sehemu ya viwanja hivyo vitatumika kufidia viwanja 2,958. Hivyo tunatarajia kumaliza changamoto hii katika mwaka wa fedha wa 2023/24,” alisema

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *