Dk Magembe: Matumizi holela ya dawa janga jipya

SERIKALI imeiasa jamii katika Bara la Afrika kuunganisha nguvu na kushirikishana katika afua mbalimbali zitakazochangia katika kukabiliana na usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa (UVIDA) kutokana na kukithiri kwa matumizi holela ya dawa za antibiotiki kwa binadamu pamoja na shughuli za ufugaji na kilimo.

Mganga Mkuu wa Serikali Dk Grace Magembe ametoa rai hiyo leo Desemba 2, 2025, Dar es Salaam wakati akizungumza na wanahabari katika maadhimisho ya Wiki ya Kukabiliana na Usugu wa Dawa na matumizi holela ya dawa kwa binadamu, mifugo na kilimo.

“Tunataka tuunganishe nguvu kutoka afua mseto za wadau mbalimbali walio mstari wa mbele kwenye vita hii na kuwa na matumizi sahihi ya dawa kulingana na maelekezo ya wataalam,” amesema Dk Magembe.

SOMA: Kampeni ya Holela-Holela itakukosti yazinduliwa

Amesema, baadhi ya tafiti zilibainisha uwepo wa matumizi holela ya dawa za binadamu kwenye mifugo na mazao, hali inayochangia dawa kutofanya kazi kwa ufanisi na kusababisha matumizi ya dawa yenye nguvu zaidi ili kutibu, hali inayochangia gharama kubwa katika matibabu na wakati mwingine husababisha madhara makubwa kwa binadamu, mifugo pamoja na mazao.

Dk Magembe ameongeza kuwa, baadhi ya watu huandikiwa dawa siku 5 hadi 7 lakini wakinywa siku ya kwanza na ya pili na kupata nafuu wanaacha hali hiyo inazidi kuongeza usugu wa vimelea vya maradhi na hata kuchochea vifo kutokana na usugu huo.

Dk Magembe amesema hatua zinazochukuliwa na serikali ni pamoja na elimu kwa wananchi mfano Kampeni ya “Holela Holela Itakukosti”, kufuatilia matumizi sahihi ya dawa na usugu, kuimarisha maabara za uchunguzi kwenye sekta ya afya na mifugo, kuzingatia njia sahihi za kupunguza maambukizi ya magonjwa (Infection Prevention Control) kwenye vituo vya tiba na kuboresha ushirikiano na uratibu wa sekta kupitia Afya Moja chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mmoja wa wawasilishaji mada katika maadhimisho hayo, Yuda Sule amesema ili malengo ya kukabiliana na usugu ya dawa yafanikiwe ni muhimu kila mmoja ndani ya jamii akaona ana wajibu wa kuchukua hatua.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button