Dk Mapana awaita wasanii BASATA

DAR ES SALAAM: Wasanii wa sanaa mbalimbali wametakiwa kujisajili katika Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa lengo la kupatiwa vibali vya kufanya kazi za sanaa.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mtendaji wa BASATA, Dk. Kedmon Mapana katika onesho la jukwaa la ‘Lady in Red’ iliyofanyika katika Ukumbi wa Warehouse, Masaki jijini Dar es Salaam.

Dk. Mapana amesema sifa moja ya kusajiliwa ni kutambulika na serikali, pia unapata fursa ya kupata mikopo.

“Wasanii, vikundi, warembo, wabunifu, wanamitindo na wachoraji mnatakiwa kujisajili kwa lengo la kufanya kazi kwa uhuru ndani na nje ya Tanzania,” amesema Mapana.

Katibu huyo aliwapongeza Kampuni ya Hugo Domingo kutumia jukwaa hilo kwa lengo la kusaidia ikiwemo kusaidia watoto ambao wamefanyiwa upasuaji wa moyo kulipa fedha za matibabu ya dawa na matumizi mengine.

“Pongezi kwa waandaji kwa sababu wameona fadhila ya kurudisha kwa jamii, pia jukwaa hili linatoa wabunifu na wanamitindo wachanga ambao miaka ya baadaye watawakilisha vyema taifa,” amesema Mapana.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Mario Fernandes alisema baada ya kukusanya fedha na kupiga hesabu ndiyo watawasilisha fedha hizo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

“Tunashukuru muitikio umekuwa mkubwa tofauti na miaka ya nyuma, pia baadhi ya watu wamechangia fedha na kuungana na sisi, milango bado ipo wazi kwa sababu bado hatujakabidhi,” amesema Fernandes.

Mbunifu Mkongwe, Mustafa Hassanali alisema, onesho la jukwaa la ‘Lady in Red’ linakuwa kila siku kutokana na wabunifu kutungeneza bidhaa zinazoendana na ukuaji wa soko.

Habari Zifananazo

Back to top button