Dk Mpango aagiza ukaguzi vituo vya mafuta

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ameiagiza Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi kushirikiana na Wizara ya Ardhi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, kufanya ukaguzi wa kina juu ya vituo vya mafuta vinavyojengwa kwa wingi kwenye makazi ya watu mkoani Dar es Salaam ili kunusuru kusitokee majanga ya moto.

Aidha, Dk Mpango ameiagiza pia Wizara ya Mambo ya Ndani kushirikiana na Wizara ya Maji kutengeneza matoleo ya maji katika maeneo mbalimbali nchini ili yawe msaada wa haraka yanapotokea majanga ya moto katika maeneo husika kwa Jeshi la Zimamoto.

Dk Mpango aliyasema hayo katika hafla ya ufunguzi wa jengo la Kituo Kikuu cha Zimamoto na Uokoaji Temeke, Dar es Salaam jana.

“Lakini kuna changamoto mbalimbali, kwa mfano hivi sasa Dar es Salaam tunashuhudia ongezeko la kujengwa vituo vya mafuta katika makazi ya watu, sidhani kama utafiti ulifanyika kwa kina kabla ya vituo hivi kujengwa, natoa rai kwenu hakikisheni taratibu za kisheria zinafuatwa na ukaguzi husika unafanyika, tusisubiri majanga yatokee tutafute mchawi,” alisema.

Vituo vya kusambaza maji Dk Mpango alisema kutokana na kukua miji kwa kasi, kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji wakati kunapotokea janga la moto, hali inayofanya gari la zimamoto kukosa maji likiwa eneo la tukio na kuagiza Wizara ya Mambo ya Ndani kushirikiana na Wizara ya Maji kujenga vituo vya maji katika maeneo mbalimbali.

“Ili kuinusuru miji yetu, ninaitaka Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi kushirikiana na Wizara ya Maji na taasisi mbalimbali kuhakikisha miradi ya maji inahusisha ufungwaji wa vituo vya maji na kuhakikisha vinakuwa na maji wakati wote kama tahadhari yanapotokea majanga,” alisema.

Huduma kwa wakati “Kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu jeshi la zimamoto kuchelewa kufika kwenye eneo la tukio kwa uokoaji na naamini hili linatokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na huduma ya zimamoto na uokoaji kuwa mbali na maeneo ya matukio… napenda kuelekeza Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kushirikiana na mamlaka za mikoa na serikali za mitaa, kutenga maeneo kwa ajili ya kujenga vituo zaidi.

“Kwa upande wa serikali kuu, dhamira yetu ni kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo katika wilaya zote nchini, ili kuhakikisha huduma inapatikana kwa haraka zaidi,” alisema. Ujenzi holela wa makazi Kuhusu ujenzi holela wa makazi, makamu wa rais alisema hiyo ni sababu nyingine inayokwamisha jeshi la zimamoto kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

“Napenda kuwakumbusha tena Wizara ya Ardhi na mamlaka zote zinazohusika kuendelea kudhibiti ujenzi holela ili kuhakikisha maeneo ya makazi yanakuwa na barabara ya kuliwezesha jeshi la zimamoto na uokoaji kufika kwenye tatizo kwa haraka na hususani wakati wa dharura,” alisema.

Matumizi ya Tehama Kuhusu matumizi ya Teknolojia, Dk Mpango alisema katika dunia ya sasa hakuna budi kwenda na wakati katika matumizi ya tehama kutatua changamoto mbalimbali kwa wananchi.

“Ni muhimu jeshi lijielekeze kuweka mifumo ya tehama ambayo itawezesha kutoa huduma za kimtandao katika ofisi za zimamoto ili kuharakisha mawasiliano kwa wananchi ili kutoa huduma haraka zaidi,” alisema.

Kuhusu jeshi hilo kujiongezea mapato ya ndani, Makamu wa rais alilipongeza jeshi hilo na kusisitiza liwe na mfumo wa kielektroniki katika kudhibiti fedha hizo.

Akizungumza mapema, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni aliishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha miundombinu na kujenga vituo vya uokoaji. Kituo hicho kilichotumia zaidi ya Sh bilioni nne, ni cha tatu kuzinduliwa katika kusherehekea kutimiza miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Aprili 16, mwaka huu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alizindua vituo kama hivyo Chamwino na Uzunguni, Dodoma. Serikali imetenga takribani Sh bilioni 10 kwa mwaka wa fedha 2023/24 kwa ajili ya ujenzi wa vituo saba maeneo mbalimbali ikiwemo Songwe, Simiyu, Kagera, Njombe, Manyara, Katavi na Geita.

Habari Zifananazo

Back to top button