MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amesema mataifa yanapaswa kuongeza uwekezaji katika sekta ya elimu ili kuhakikisha watoto wanapata elimu bora na ya uhakika.
Dk Mpango alisema hayo jijini New York nchini Marekani alipohutubia Mkutano wa Umoja wa Mataifa (UN) uliobeba ajenda ya mageuzi katika sekta ya elimu ulioshirikisha wakuu wa nchi na serikali, wakuu wa taasisi na mashirika na wadau wa elimu.
Yupo nchini Marekani kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa (UNGA).
Dk Mpango alisema elimu ni sehemu muhimu ya Ajenda ya Maendeleo 2030 hivyo ni muhimu kuchukua hatua ili kuleta mabadiliko kwenye sekta hiyo kwa kuwa ikipatikana elimu bora itapunguza matabaka katika ajira na kipato baina ya wananchi.
Alisema Tanzania imechukua hatua kuboresha sekta ya elimu ikiwamo kuanza mchakato wa kuboresha mitaala kwa kuwashirikisha wadau wa elimu, kuwekeza katika vyuo vya ufundi stadi na mafunzo, kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari na kuongeza bajeti ya wizara husika kufikia asilimia 18 ya bajeti yote ya serikali.
Alisema serikali imedhamiria kuboresha usimamizi wa nguvu kazi ya walimu ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji bora kwa kuwajengea uwezo walimu na maofisa elimu kuhusu uunganishaji wa teknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji na uandaaji wa masomo ya kidijiti.
Dk Mpango alisema Serikali ya Tanzania inahakikisha upatikanaji wa elimu jumuishi kwa wote bila kujali jinsi, ulemavu na hali ya uchumi.
Awali, alipozungumza na diaspora wa Tanzania waliopo katika miji ya New York, Connecticut na New Jersey, aliwasihi waendelee kuchangia maendeleo ya nchi yao.
“Muendelee kujishughulisha na shughuli za uwekezaji nchini kwani kufanya hivyo mnachangia maendeleo ya nchi yenu, mnaiunga mkono serikali katika jitihada za kuleta maendeleo kwa watu wake,” alisema Dk Mpango.
Aliwasihi wanadiaspora hao wafuatilie na kutumia fursa zilizopo nchini kwa manufaa yao, ndugu na jamaa na taifa lao kwa ujumla.
Aliwapongeza diaspora wa Tanzania kwa kuendelea kutoa mchango wa uwekezaji hasa kupitia Mfuko wa UTT Amis, akisema hadi kufikia mwaka 2021 walikuwa wamewekeza zaidi ya Sh bilioni 3.9.