MAKAMU wa Rais Dk.Philip Mpango amekemea tabia ya wanaume wanaipiga wake zao na kwamba tabia hiyo imechangia kuongezeka kwa watoto wanaozaliwa ambao hawajatimiza umri wa kuzaliwa (watoto njiti).
Dk.Mpango amesema hayo wilayani Buhigwe mkoani Kigoma, alipokuwa akipokea misaada mbalimbali iliyotolewa na taasisi ya Doris Mollel Foundation na Tume ya Ushindani (FCC) kwa ajili ya kusaidia kukabili changamoto ya watoto njiti kwenye hospitali ya Wilaya Buhigwe mkoani Kigoma.
Amesema tabia hiyo haikubaliki hata kidogo, kwani pamoja na athari ya kiafya kwa wanawake wajawazito wanaopigwa, lakini imesababisha msongo wa mawazo kwa wanawake hao hivyo kuzaa watoto ambao hawajatimiza umri.
Amesema kitendo cha Doris Mollel kuanzisha mpango wa kusaidia changamoto ya watoto njiti haina budi kuungwa mkono na watu wote na kuwataka wakuu wa wilaya,wakurugenzi wa halmashauri na waganga wakuu wa wilaya kutengeneza mipango ambayo itawawezesha kusaidia tatizo hilo.
Katika mpango wa kusaidia watoto njiti, Makamu wa Rais ameipongeza taasisi ya SamaKiba kwa mechi ya hisani iliyofanyika, ambapo fedha zilzopatikana zimesaidia sehemu ya msaada huo.
Akizungumza wakati akikabidhi vifaa kwa Halmashauri ya wilaya Buhigwe, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC,Monica Moshi alisema kuwa tume hiyo imekabidhi vifaa tiba kwa ajili ya sekta ya afya kwenye vituo vya afya vilivyopo pembeni ya wilaya ya Buhigwe hususani vya kudhibiti vifo vitokanavyo na uzazi.