MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amewataka wananchi wa Kanda ya Ziwa kutumia shamba la mifugo Mabuki, lililopo wilayani Misungwi mkoani hapa, kwa ufugaji wenye tija.
Shamba hilo ni maalum kwa uzalishaji wa mifugo ya kisasa, hasa ng’ombe, wa kutoa mazao mengi na bora.
Ametoa wito huo leo April 11, 2023, aliposimama kuwasalimia wananchi wa Kata ya Hungumalwa Wilayani Kwimba, akitokea mkoa wa Shinyanga.
Alisema shamba hilo ni kwa ajili pia ya kusambaza elimu kwa wananchi kuacha ufugaji wa zamani, wenye idadi kubwa ya ng’ombe lakini hawana faida.
“Mifugo iliyopo si bora ambayo taifa linahitaji. Tubadilishe aina ya mifugo sasa ,”ameshauri.
Baada ya kuzungumza na wananchi, Dk Mpango ametembelea shamba hilo na kuelezwa kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ametoa mitamba 500 kwa ajili ya uzalishaji wa mifugo bora itakayosambazwa kwa wananchi.
Meneja wa shamba, Lini Mwalla, ameeleza baada ya uzalishaji, ng’ombe bora watauzwa kwa wananchi kwa bei ya ruzuku, ambayo ni Sh million mbili kwa jike ambaye tayari ana mimba, na Sh millioni moja kwa dume.
Sambamba na hilo, wataalam Mabuki pia wanazalisha malisho yenye virutubishi vyote muhimu pamoja na mbegu zake, kwa uhakika wa chakula kwa mifugo hiyo ya kisasa.
“Tunawatembelea wafugaji kuwapatia elimu kwa vitendo,” amesema.
Mwalla alizungumzia changamoto mbalimbali zinazolikabili shamba hilo, ikiwemo uvamizi wa mifugo ya wananchi.
Mojawapo ya athari za uvamizi huo ni ng’ombe wa asili kuingiliana na wale wa mbegu ya kisasa, hivyo kuharibu ubora wa kizazi kilichokusudiwa, alisema.
Katika shamba hilo, Makamu wa Rais, akashauri ufugaji bora uhusishe, pamoja na mambo mengine, uwepo wa maofisa ugani karibu na wafugaji, huku kila mmoja akiwa na idadi ya mifugo anayohudimia.