Dk Mpango atoa maagizo utekelezaji miradi

UTEKELEZAJI duni wa miradi ya maendeleo inayofanyika katika wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, imemkera Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango na kuiagiza Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa Kigoma kumpatia haraka taarifa ya miradi waliyotembelea na kukagua kwa mkoa Kigoma aipitie na kuchukua hatua.

Akizungumza wilayani Buhigwe akiwa kwenye siku ya tatu ya ziara ya kiserikali mkoani Kigoma, Makamu wa Rais amesema kuwa anazo taarifa za baadhi ya miradi utekelezaji wake haifanani na fedha zilizotolewa kwa ajili ya miradi hiyo na kwamba hawezi kukubaliana na hali hiyo, ni lazima waliosababisha wawajibishwe.

Ametoa mfano wa soko la Kimataifa la Mnanira lililopo Mpakani na nchi ya Burundi na kusema kuwa taarifa alizonazo kuhusu utekelezaji wa soko hilo haumridhishi na kutaka apatiwe taarifa nzima ya mradi huo.

Amemuagiza Mwenyekiti wa CCM Mkoa Kigoma, Jamal Tamim na Mkuu wa Mkoa Kigoma,Thobias Andengenye kumpatia taarifa za miradi waliyokuwa wakitembelea na kukagua haraka, ili aweze kuchukua hatua.

“Serikali imeleta fedha nyingi mkoani Kigoma kwa ajili ya utekelezaji wa miradi kuleta maendeleo kwa wananchi, kuondoa kero na kuboresha maisha yao, lakini kuna watu wamepewa mamlaka ya kusimamia miradi hiyo wanafanya wanavyotaka wao na miradi haiko kwenye hali ambayo serikali inataka, mingine ipo wilayani kwangu nilipozaliwa, hiyo haiwezekani, lakini niondoke na kichwa cha mtu wanaofanya mchezo na miradi hiyo,” amesema Makamu wa Rais.

Akizungumza katika mkutano huo kwenye Hospitali ya Wilaya ya Buhigwe Mkuu wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye amesema kwa mwaka wa fedha uliomalizika Juni, 2023,  serikali imeleta  mkoani Kigoma kiasi cha Sh Bilioni 38.1 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya afya, ambapo kiasi cha Sh bilioni 35.2 sawa na asilimia 92.4 zimeshatumika kwenye utekelezaji wa miradi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa Kigoma, Jamal Tamim ameipongeza serikali kwa kutoa fedha nyingi mkoani humo na kutekeleza miradi ya kimkakati, hivyo kupitia kamati ya siasa wako macho kuangalia utekelezaji wa miradi hiyo inatekelezwa kikamilifu kama ilivyopangwa, na kwamba watatumia nafasi yao katika usimamizi wa ilani kutoa taarifa za hali ya miradi na kutoa taarifa kuhusu wasimamizi wasiotekeleza wajibu wao wawajibishwe.

Habari Zifananazo

3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button