Dk Mpango atoa maagizo utekelezaji miradi

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amewataka wenyeviti wa halmashauri na mameya wa majiji wasimamie utekelezaji wa miradi ya maendeleo itekelezwe kwa viwango.

Aidha, Dk Mpango amewaagiza viongozi hao waepuke rushwa na ufujaji wa fedha za miradi ili wananchi wapate huduma bora na waone matokeo ya fedha za kodi wanazozitoa kwa serikali.

Alitoa maagizo hayo jana jijini Mbeya alipofungua Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) unaohudhuriwa na wenyeviti wa halmashauri za wilaya, miji na mameya wa majiji nchini.

Advertisement

Dk Mpango alisema serikali imekuwa ikitekeleza miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu na barabara kwenye halmashauri zote kwa kutumia fedha zinazotokana na vyanzo mbalimbali.

Alisema baadhi ya wasimamizi wa miradi hiyo wamekuwa wakizichepusha fedha na kuzitumia kwa maslahi yao.

“Kwenye halmashauri zetu bado kuna mchwa wanaotafuna fedha, fedha zinatengwa kwa ajili ya miradi lakini wao wanazichepusha na kuziingiza kwenye mifuko yao binafsi, nawaombeni sana ninyi mlioaminiwa fanyeni kazi kwa uadilifu,” alisema Dk Mpango.

Alisema yeye ni miongoni mwa viongozi ambao wamekuwa wakitafsiriwa kwamba ni wapole lakini huwa si mvumilivu kwa yeyote anayefuja mali za umma.

Dk Mpango alisema ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyoishia Juni 30, 2021 ilionesha kuwa baadhi ya halmashauri zilipata hati chafu na asilimia 17 ya halmashauri zilishindwa kurekebisha kasoro ama kujibu hoja za ukaguzi.

“Pia ripoti hiyo ya CAG ilionyesha kuwa kulikuwa na dosari kwenye manunuzi ikiwemo manunuzi yaliyofanyika bila ushauri wa Bodi za wazabuni, ununuzi ambao haukufuata utaratibu wa kushindanisha wazabuni na fedha kutorejeshwa na wakandarasi baada ya mikataba kuvunjika,” alisema Dk Mpango.

Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Murshid Ngeze alisema lengo la jumuiya hiyo kwa mwaka huu ni kuongeza ukusanyaji wa mapato kwenye halmashauri na majiji na kusimamia matumizi ya mapato hayo kwenye utekelezaji wa miradi.

Ngeze alisema mamlaka za serikali za mitaa zimekuwa zikifanya kazi nzuri lakini zinakabiliwa na changamoto yakiwemo malipo kidogo kwa madiwani na wakurugenzi.