MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amelitaka Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) kubuni mbinu mpya za kuchagiza agenda ya kuifanya Tanzania kuwa ghala la chakula katika Ukanda wa Afrika na pande zingine za dunia.
Pia alisisitiza haja ya Jeshi hilo kuwekeza katika matumizi ya teknolojia kwenye uzalishaji mali na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Dk Mpango alisema hayo jana jijini hapa wakati wa kuzindua wiki ya maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa jeshi hiyo, Julai 10 mwaka 1963.
Alisema ana imani kuwa JKT inaweza kuwa chachu ya kuifanya Tanzania kuwa ghala la chakula.
Dk Mpango alisema ili kufikia adhma hiyo aliitaka JKT kuwekeza zaidi katika kufundisha vijana matumizi ya teknolojia katika shughuli zao mbalimbai za uzalishaji mali na utoaji huduma kwa wananchi.
“Zama hizi sio za kutumia misuli, bali kutumia akili zaidi na teknolojia zaidi na katika hili ni vyema Jeshi la Kujenga Taifa lifikirie namna ya kuwatambua wataalamu wake wabunifu na kuwapatia tuzo na kuwa na hakimiliki za utaifiti na ugunduzi,”alisema.
Dk Mpango pia alisisitiza na kuikumbusha JKT kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake katika uhifadhi na utunzaji wa mazingira, upandaji wa miti katika makambi yote na utunzaji vyanzo vya maji.
Aliwataka pia kuunga mkono udhibiti wa taka za plastiki ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira na kuhimiza matumizi ya nishati safi ili kupunguza ukataji miti na hivyo kuchangia juhudi za uhifadh wa mazingira.
Aidha, Dk Mpango alisema anatambua mchango adhimu wa JKT katika kuwalea, kuwajenga nidhamu, maadili mema, uzalendo, ukakamavu na kuwafundisha ujuzi mbalimbali vijana na kuwafanya sehemu ya maendeleo ya kiuchumi na ulinzi wa Taifa.
Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa alisema JKT imeendelea kuwa chombo imara cha kuwapatia vijana ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa na kuwa chombo imara cha huduma na uzalishaji mali hasa katika ujenzi, kilimo na uvuvi.
Awali Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele alisema miaka 60 ya kuanzishwa kwa jeshi hilo limeweza kutekeleza majukumu yake kwa mafanikio makubwa ikiwemo kubadili fikra za vijana katika malezi na maadili kwa ustawi bora wa maendeleo ya nchi.