Dk Mpango mgeni rasmi siku ya misitu duniani

MAKAMU wa Rais wa Tanzania, Dk Phillip Mpango atarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Siku ya Upandaji Miti Kitaifa yanayotarajiwa kufanyika Machi 21, 2024.

Kuelekea siku hiyo, WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki amekagua mabanda ya maonesho yatakayotumika katika maadhimisho hayo.

Akitembelea mabanda yaliyopo kwenye maonesho hayo, Kairuki ameipongeza wizara pamoja na wadau wa misitu waliojitokeza kutoa elimu kuhusu majukumu yanayotekelezwa na taasisi zao ikiwemo elimu ya uhifadhi pamoja na kuonesha bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na mazao ya misitu.

Aidha, Kairuki ametumia fursa hiyo kuwataka wakazi wote wa Wilaya ya Same, Mkoani Kilimanjaro pamoja na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kutembelea maonesho hayo.

Amesema maonesho hayo ni muhimu kwani wataweza kujifunza masuala mbalimbali ikiwemo elimu ya ufugaji nyuki kibiashara pamoja na kujua fursa mbalimbali zinazopatikana katika mnyororo wa thamani ya mazao ya misitu.

Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Siku ya Upandaji miti Kitaifa hufanyika kila mwaka Machi 21 ambapo kwa mwaka huu Tanzania inaadhimisha kilele hicho kwa kupanda miti pamoja na kutembelea maonesho ya bidhaa mbalimbali zitokanazo na misitu na nyuki.

Habari Zifananazo

Back to top button